MH. PINDA AHUDHURIA IBADA YA KUMWEKA WAKFU ASKOFU WA
MORAVIAN JIMBO LA RUKWA
*Ataka viongozi wa dini wasichoke kuombea
amani ya Taifa
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaendelea
kusimamia msimamo wake wa kutokuwa na dini wala nchi kutokuwa na dini lakini
itaendelea kuruhusu watu wawe na dini zao.
Ametoa
kauli hiyo jana mchana Jumapili, Mei 25 kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu
Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa
iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko
nje ya nchi kikazi, alisema:
“Leo
tukiruhusu Serikali iwe na dini na tayari katika dini zote kuna makundi madogo
madogo, je wale wa upande mwingine utawaacha wapi?”.
Pia
alitumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wa dini nao pia waangalie wasitumbikie
kwenye mtego wa siasa na kuruhusu kanisa zima liwe la chama fulani kwani miongoni
mwa waumini wao wapo pia wapenzi wa vyama vingine.
“Kama
mtu binafsi, kiongozi wa dini anaweza kuwa mpenzi wa chama lakini kama Kanisa
tusiruhu hali hiyo,” alionya.
Aliwaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na hasa waombee amani ya Taifa
hili.
“Ninawasishi
viongozi wa dini msichoke kuombea amani ya Taifa hili kwani amani ikipotea kama
nchi hatuna mahali pa kukimbilia.
MZINDAKAYA
AGOMA KUMSAMEHE MBUNGE WA SUMBAWANGA MJINI...
Mbunge wa
zamani wa jimbo la Kwela, Mzee Chrisant Mzindakaya (shoto) amekataa kumsamehe
hadharani Mbunge wa sasa wa Sumbawanga Mjini, Bw. Aeshi Hilali (kulia) baada ya
kupewa fursa ya kushikana mikono jukwaani na kusameheana.
Haya yametokea leo mchana
(Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad
Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa iliyofanyika kwenye
Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.
Mzee
Mzindakaya alikataa kufanya hivyo akisema yeye ni mkristu lakini hakuwa
ameandaliwa kiroho kwa ajili ya tukio hilo. “Hapa ni shughuli ya kanisa na si
mkutano wa Chama. Lazima niwe mkweli leo sijajiandaa kwa jambo hili… Mimi ni
mtu mzima, nafsi ya msamaha inahitaji maandalizi, nahitaji maandalizi ya
kiroho,” alisema.
Hata hivyo,
alikiri kwamba amekubali msamaha alioombwa na Bw. Aeshi lakini hawezi kuutoa
katika shughuli ya Kanisa. “Nilishamwambia Mwenyekiti wa CCM mkoa aitishe
mkutano, wazee wa chama wawepo na sisi wawili tuwepo kwa sababu nimetukanwa
sana kama vile sijaifanyia jambo lolote nchi hii,” alisisitiza.
“Niliwaeleza
pia waandae mikutano ya nje kule kwa wanachama ambako nilichafuliwa sana.
Nikisema nimemsamehe hapa nitakuwa mnafiki,” aliongeza.
Kwa
upande wake, Bw. Aeshi ambaye alipewa nafasi ya kwanza kuomba msamaha, alisema
anatambua kwamba bega haliwezi kukizidi kichwa na yeye kama mtoto anamuomba
msamaha Mzee Mzindakaya kwa yaliyopita ili waweze kufanya kazi pamoja na kuleta
maendeleo kwa wakazi wa jimbola Sumbawanga Mjini.
“Natambua
kuwa mimi ni mtoto na siku zote mdogo atabaki kuwa mdogo lakini naomba busara
zake ili tushirikiane kuleta maendeleo ya mkoa wetu… yaliyopita si ndwele
tugange yajayo. Nimetamka maneno haya mbele ya viongozi wa dini na mbele ya
Mungu kwa kuwa najua yuko hapa,” alisema.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya ndiye aliwaomba Mzee Mzindakaya na
Bw. Aeshi wapande jukwaani na kupeana mikono na kisha akawapa kila mtu fursa ya
kutoa neno.
Mhandisi
Manyanya alisema siku ya leo ni ya kipekee na akaona asipoteze fursa hiyo bali
aitumie kuwaomba viongozi hao ambao wamekuwa na uhasama wa muda mrefu
wayamalize kwa kupeana mikono hadharani.
POLISI
WAUNGANISHA NGUVU KUKABILIANA NA UHALIFU MTANDAO
Polisi wa visiwa vya kifalme vya Solomon vilivyopo pasifiki ya kusini
wameunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya uhalifu mtandao na kuelezwa ya
kwamba nguvu kubwa itasogezwa mashuleni ili kukuza uelewa wa maswala ya uhalifu
mtandao (Awareness) na kusisitizwa hiyo ndio itakua shabaha yao ya awali.
Hayo yamebainishwa na Bradford Theonomi Kupitia program ya mpango
uliopewa jina la “Cyber safety pasifika” uliopangwa kuwasaidia watoto, vijana
na wakubwa kutumia teknolojia katika hali ya usalama iliyojiri kuanzia mnamo
tarehe 19 -25 May mwaka huu (2014) ulilenga kuhakiki matumizi salama ya
mitandao visiwani humo unapewa kipaumbele na ukanda mzima wa pasifiki ya kusini
kwa ujumla wake.
Makubaliano
hayo yalifikiwa wakati wa mkutano ulio fanyika na kuwahusisha wakuu wa polisi
wa visiwa hivyo. Kauli mbiu iliyo someka kama “ Historia yetu, Utamaduni wetu
na mitandao yetu” Ilidahmiriwa kuhamasisha matumizi salama ya mitandao na simu
katika ukanda huo wa pasifiki ya kusini.
Bi. Juanita
Matanga, Mkuu wa polisi wa visiwa hivyo aliainisha utayari wa kujipanga
kukabiliana na uhalifu mtandao huku akitolea maelezo ukuaji wa kasi wa matumizi
ya mitandao na simu katika visiwa hivyo na duniani kwa ujumla.
Aidha Alieleza ukuwaji wa matumizi ya mitandao bahati mbaya wengi
hawajui athari zake. Hilo ndilo lililo wasukuma kuanzisha kampeni hiyo ya
kukuza uelewa wa maswala ya uhalifu mtandao (Cybercrime Awareness Campaign)
visiwani humo.
Matanga
alisisitiza kampeni hiyo itakua endelevu na pia kutakua na kupitia sharia
zilizopo ili kuweza kuziboresha kuhimili makosa ya uhalifu mtandao.
Alianisha pia katika visiwa
hivyo bado ukuaji wa kasi wa makosa ya kimtandao haujaanza kuonekana na polisi
visiwani humo wako katika kuhakiki wanakuza uelewa kwa raia wake ili kuweza
kukabiliana na hali hiyo – Kuzuia tatizo ni bora zaidi kuliko kusubiri tatizo
litokee ili kuanza kukabiliana nalo.
Mkuu huyo wa
polisi alianisha pia yakua nchi nyingine za ukanda huo wa pasifiki tayari
wamesha kua na taratibu wa kuhamasisha matumizi bora ya mitandao kukabiliana na
uhalifu mtandao (Cybercrime awareness programs) na umefika wakati visiwa
hivyo navyo kuingiza taratibu hiyo katika vitendo na kusisitiza tena kua swala
hilo litakua endelevu.
MELI ZA JESHI LA UTURUKI NCHINI KUTIA NANGA DAR ES
SALAAM
Ziara ya Meli za Jeshi la Uturuki Nchini Tanzania.
Meli Nne za Kijeshi za Uturuki kwa jina la Barbaros Turkish Maritime Task Group
(TMTG) zinatarajiwa kutia nanga kwa wakati mmoja katika Bandari ya Dar es
Salaam kwa ziara ya kijeshi ya siku 4 ambao itahusisha maonyesho ya zana za
kijeshi, mazoezi ya pamoja na jeshi la wanamaji la Tanzania, huduma za kijamii
na ushirikiani wa kijeshi baina ya Uturuki na Tanzania.
Hayo yamebainishwa jiji Dar es Salaam na Balozi wa Uturuki nchini, Ali
Dovitoglu katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika Ubalozi wa
Uturuki, jijini Dar es Salaam.
Balozi Dovitoglu amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kukuza ushirikiano
wa kijeshe baina ya jeshi la Uturuki na majeshi ya nchi 27 za pwani barani
Afrika sio tuu kuonyesha uwepo na uwezo wa kijeshi wa Jeshi la Wanamaji la
Uturuki, bali pia kusaidia katika operetions mbalimbali za kijeshi barani
Afrika ukiwemo vita dhidi ya uharamia kwa Pwani ya Bahari ya Hindi.
Balozi Dovitoglu amesema meli hizo zitawasili siku ya Jumanne tarehe
27/05/2014, Siku ya Jumatano, tarehe 28/05 2014 waandishi wa habari
watakaribishwa kufanya ziara katika meli hizo, baadaye wanamaji hao,
watatembelea shule na kituo cha watoto yatima kugawa misaada ya
kibinaadamu.
Siku ya Alhamisi na Ijumaa, wananchi wa jiji la Dar es Salaam na
vitongoji vyake, wataruhusiwa kutembelea meli hizo kwa muda wa siku 2 kuanzia
saa 3 asubuhi mpaka saa 6 mchana kujionea maonyesho ya zana za kijeshi ya
Uturuki ambapo makampuni manane ya vifaa vya kijeshi ya Uturuki wataonyesha
vifaa vyao.
Makampuni hayo ni Meteksan, Otokar, TAI, Dearsan, Havelsan, Roketsan,
Aselsan na STM
Meli hizo nne ni F-495 TCG kwa jina la Gediz, F-245 TCG, Oruçreis,
F-511 TCG Heybeliada meli ya usindikizaji ya A-595 TCG Yarbay Kudret Güngör,
zitasafiri kwa jumla ya safari ya urefu wa kilometa 30,000 katika ziara
itakayochukua siku zaidi ya 100 ambapo itatembelea nchi 28 barani Afrika na
kutia nanga katika bandari 40.
Msafara wa meli hizo, unaingia Tanzania ukitokea nchini Afrika ya
Kusini, ambapo hii ni mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka 148 iliyopita
ndipo meli ya mwisho ya Uturuki ilitia nanga kwa mara ya mwisha katika Rasi ya
Tumaini Jema (Cape of Good Hope) mwaka 1866.
Uturuki ni moja ya mataifa makubwa yenye nguvu kubwa za kijeshi
la la majini, tangu enzi za utawala wa kale wa dola la Ottoman ambapo
walitawala bandari nyingi barani Afrika ikiwemo miji ya Kilwa, Sofala, na Lamu
kwatika Pwani ya Bahari ya Hindi.
KURA KUHESABIWA UPYA LEO NCHINI MALAWI.
Nchini Malawi kura za uchaguzi
mkuu zinatarajwa kuhesabiwa upya hii leo katika maeneo ambapo imedhihirika kuwa
idadi ya wapiga kura haiwiani na idadi ya wale waliojiandikisha kupiga kura.
Uchaguzi mkuu wa Malawi umezidi kuchukua sura
mpya baada ya wanasiasa na wanasheria nchini humo kupeleka malalamiko yao
mahakamani, na kuzidi kuchelewesha matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika jumanne
iliyopita.
Kulingana na mwandishi wa idhaa ya Kiswahili
ya BBC aliye mjini Lilongwe, Baruan Muhuza, hali nchini humo imekuwa ya
sintofahamu ambapo hakuna ye yote anayejua uchaguzi utaishia wapi.
Anasema kuwa tume ya uchaguzi imekiri kuwa
kuna maeneo kadhaa ambayo kuhesabu kwa kura kutarudiwa kwa sababu kura
zilizopigwa zinazidi waliojisajili.
" Tume ya uchaguzi inasema kuwa kuna
maeneo mengine ambako watu wamepiga kura mara tatu au mara nne kama vile mji wa
Mangochi waliosajiliwa ni watu 39,000 pekee lakini kura zilizopatikana hapo ni
180,000," Baruan alisema.
AU: KUTEKWA NYARA
WANAFUNZI KUNAKINZANA NA UISLAMU
Rais Muhammad Ould Abdulaziz wa Mauritania ambaye
pia ni Mwenyekiti wa mzunguko wa Umoja wa Afrika, amesema kuwa kitendo cha
kutekwa nyara zaidi ya wanafunzi wa kike 200 na kundi la Boko Haram nchini
Nigeria, kunakinzana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Rais Muhammad
Ould Abdulaziz ameyasema hayo katika ujumbe alioutoa kwa watu wa bara la Afrika
katika sherehe za kuadhimishwa miaka 51 ya kuasisiwa Muungano wa Nchi Huru za
Afrika OAU.
kabla ya
kubadilishwa na kuitwa Umoja wa Afrika AU, ambapo pamoja na mambo mengine
amelaani vikali kitendo hicho na kutaka wanafunzi hao waachiliwe huru mara moja
na bila ya masharti yoyote.
Mwenyekiti
huyo wa mzunguko wa Umoja wa Afrika ameongeza kuwa, hali ya mambo nchini Mali,
Nigeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Somalia, Sudan Kusini na Libya, ni
changamoto kubwa kwa umoja huo na hivyo amezitaka pande hasimu katika nchi hizo
kumaliza tofauti zao ili kudhamini usalama na maendeleo kwa wananchi wao.
Kwa upande
mwingine Rais Muhammad Ould Abdulaziz amekutaja kujitosheleza katika chakula,
kustawisha biashara ya bidhaa za kilimo, kupambana na umasikini na lishe duni
kuwa mambo yanayopewa kipaumbele na Umoja wa Afrika.
MAGAIDI WA KIKRISTO WAUA VIJANA
WAISLAMU CAR
Msemaji wa Jumuiya ya Waislamu katika Jamhuri
ya Afrika ya Kati amesema, wanamgambo wa Kikristo nchini humo wamewaua vijana
watatu Waislamu na kukatakata viungo vyao vya mwili.
Othman
Abakar, msemaji wa Jumuiya ya Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameongeza
kuwa, vijana hao Waislamu wameuawa mjini Bangui wakati walipokuwa
wakijitayarisha kuenda kutazama mechi ya mpira.
Imearifiwa kuwa mechi hiyo ilikuwa baina ya
vijana Waislamu na Wakristo kwa lengo la kuleta amani na maelewano baina ya
Waislamu wa kundi la Seleka na wanagamabo wa Kikrsito wa kundi la Anti Balaka.
Msemaji huyo wa Waislamu ameongeza kuwa miili
ya vijana hao waliokuwa wakaazi wa mtaa wa PK5 katika mji mkuu Bangui imezikwa
katika msikiti mmoja mjini humo.
Hayo
yanajiri katika hali ambayo msemaji wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka
Sebastien Wenezoui amedai kulaani mauaji hayo na kuongeza kuwa vijana wengine
10 Waislamu wametekwa nyara katika tukio hilo.
Amesema
ukatili huo umetekelezwa na vijana wa Kikristo kutoka mtaa wa Boy-Rabe mjini
Bangui.
Hayo
yanajiri katika hali ambayo siku ya Jumamosi kuliripotiwa mapigano makali baina
ya wanajeshi wa Ufaransa na Waislamu watiifu kwa kundi la Seleka katika mji wa
Bambari.
Wanajeshi wa Ufaransa wajulikanao kama
Sangaris wamekuwa wakiwashambulia Waislamu na kupuuza ugaidi unaofanywa na
wanamgambo wa Kikristo.
KARZAI AKATAA
KUKUTANA NA OBAMA MJINI BAGRAM
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amekataa
ombi la Rais Barack Obama wa Marekani la kukutana naye katika uwanja wa Jeshi
la Anga la Marekani mjini Bagram nje kidogo ya Kabul, mji mkuu wa Afghanistan.
Siku ya Jumapili rais wa Marekani aliwasili
Afghanistan katika safari ya kushtukiza na kukataa kuenda Kabul kukutana na wakuu
wa serikali ya Afghanistan.
Afisa
wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema ni kweli Karzai alialikwa
kukutana na Obama lakini aliktaa. Imearifiwa kuwa Karzai alisema yuko tayari
kukutana na rais wa Marekani katika Ikulu ya Rais mjini Kabul na si katika
uwanja wa ndege za kijeshi wa Bagram. Uhusiano wa Kabul na Washington
umevurugika kufuatia hatua ya Rais Karzai kukataa kutia saini mkataba wa
usalama na Marekani. Mkataba huo ungeiruhusu Marekani kuendelea kubakisha
vikosi vyake Afghanistan hata baada ya kumalizika muhula wa mwaka huu wa 2014
ambapo Marekani inatakiwa kuwa imeviondoa vikosi vyake vyote Afghanistan. Akiwa
katika safari yake hiyo ya kushtukiza nchini Afghanistan, Obama amesema
Marekani itamaliza oparesheni zake Afghanistan mwaka huu lakini akaongeza kuwa
Washington itabakisha vikosi vyake nchini humo.