WAZIRI
MKUU: OMBEENI TAIFA NA UCHAGUZI MKUU UJAO - ASKOFU NIWEMUGIZI ATAKA UKAWA
WARUDI BUNGENI MWEZI UJAO, ASEMA SIYO OMBI.
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini kote nchini na wananchi waungane
pamoja ili kuombea uchaguzi mkuu wa viongozi wakuu wa Rais, wabunge na madiwani
unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Ametoa wito
huo leo mchana (Jumanne, Julai mosi, 2014) wakati akizungumza na maelfu ya
waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya Jubilei ya miaka 25 ya
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarsicius Ngalalekumtwa
katika uwanja wa Kichangani wa Kanisa Kuu la Kihesa.
"Maaskofu
wote mliopo hapa, najua mnavyoipenda Tanzania... kila kanisa lina sala maalum
ya kuliombea Taifa na viongozi wake, ninawaomba viongozi wetu mliombee Taifa
letu ili mambo yaende salama na hasa uchaguzi wa mwakani," alisema.
Akirejea
mahubiri yaliyotolewa kwenye ibada hiyo na Mhashamu Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa
Jimbo Katoliki la Tabora ambaye alitoa mfano wa Daudi na Goliathi, Waziri Mkuu
alimfananisha Goliathi na masuala ya rushwa, ubinafsi na tabia ya viongozi
kutojali wananchi wa hali ya chini.
"Viongozi
tusipokuwa waadilifu, tukawa wala rushwa na hatujali wananchi wa hali ya chini
tutakuwa sawa na Goliathi. Nawasihi sana ombeeni Taifa hili na uchaguzi mkuu
ujao ili Mungu atupe Daudi atakayeweza kuliongoza Taifa hili na kulipeleka
kunakostahili," alisema huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu
ambaye alihudhuria sherehe hizo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, ametumia
fursa hiyo pia kuwaomba wote kwa pamoja waendelee kuliombea Taifa katika
kipindi hiki cha mchakato wa kuandaa Katiba Mpya. "Watanzania wote tuwe na
moyo wa kuvumiliana na kupendana. Tumuombe Mungu atuwezeshe kupata Katiba mpya
katika hali ya maelewano na amani. Tuombee Taifa na tuombee Watanzania ili
tusije tukatoka katika mstari."
Alisema
ushauri uliotolewa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severini Niwemugizi wa
kuwataaka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba warejee mara moja ni wa muhimu.
"Ushauri wa Baba Askofu ni wa makini, turudi tukabishane pale ndani,
lakini pamoja na yote sheria inasema mwamuzi wa mwisho ni Watanzania kupitia
kura ya maoni. Wale tuliopewa dhamana ya kupitia rasimu turudi pale
tuikamilishe ili Watanzania waweze kupata fursa ya kupiga kura ya maoni,"
alisema.
Mapema, akiwasilisha
salamu kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini
Niwemugizi wa Jimbo la Ngara aliwataka wajumbe wa Bunge maalum la Katiba
kurejea kwenye mkutano wake uliopangwa kuanza Agosti 5, mwaka huu.
"Ninatumia
neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee bungeni mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au
kufanya mizengwe mingine na kutupatia Katiba isiyotufaa, nitawaomba Watanzania
wote tuweke uzalendo mbele na kuikataa rasimu ya Katiba itakayoletwa na pia
tuwanyime uongozi katika uchaguzi mkuu ujao," alisema.
Aliwataka
Watanzania wajitokeze kwa wingi wakati wa kujiandikisha kwenye daftari la
wapiga kura. "Watanzania tuna tabia ya kudharau siasa. Tusidharau masuala
ya siasa kwa sababu ni muhimu na yanagusa maisha yako na yangu, yanagusa maisha
ya watoto wako," alisema.
Sherehe
hizo za jubilei ya miaka 25, zilihudhuriwa na maaskofu 19 kutoka majimbo
mbalimbali ya kanisa katoliki hapa nchini, wawakilishi wa maaskofu watatu na
abate mmoja. Viongozi wa kitaifa waliohudhuria ni Spika wa Bunge, Mama Anne
Makinda; Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa; Waziri Mkuu
mstaafu, Edward Lowassa na baadhi ya wabunge wa mkoa wa Iringa.
FILIKUNJOMBE AWAHAKIKISHIA UMEME
WANANCHI WA LIPINGU KABLA YA KRISMASS.
MBUGE
wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe ageuka mbogo kwa wale wenye nia
ya kukwamisha maendeleo jimboni awahakikishia wananchi
wa kata ya Lupingu kupata umeme kabla ya Krismass
na kuwa zoezi la kuanza kuchimba mashimo ya kuweka
nguzo za umeme litaanza jumatatu likiongozwa nay eye
mwenyewe .
Huku akiwataka
wananchi wa kata ya Lupingu kutomchagua diwani
wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 iwapo atashindwa
kushiriki kikamilifu katika usimamizi na ushiriki wa maendeleo
katika mradi huo.
Mbunge
Filikunjombe alitoa ahadi hiyo iliyopokelewa kwa
shangwe kubwa na wananchi wa vijiji vitatu vya kata ya
Lupingu leo wakati alipoongozana na wataalam wa shirika la ugavi wa
umeme nchini (TANESCO) katika vikao vya pamoja na viongozi wa serikali
za mitaa na uongozi wa wilaya na ule wa Tanesco mkoa na
wilaya ya Ludewa .
Alisema
kuwa amelazimika kupigania umeme katika vijiji mbali mbali
vya jimbo la Ludewa kama sehemu ya kuwakumbuka wananchi wake
na kuongeza idadi ya vijiji vya jimbo hilo la Ludewa kuwa na
umeme kutoka kijiji kimoja alichokikuta wakati akiingia madarakani
hadi vijijini zaidi ya 10 sasa ambavyo vina uhakika wa
kupata umeme na baadhi tayari vimepata umeme tayari .
Hivyo
alisema itapendeza kuona wananchi na vijiji vyote vya
kata ya Lupingu ambavyo ni pamoja na Nindi ,Ntumbati na Lupingu kupata
umemne kabla ya sikukuu ya krismasi na kuwa akiwa kama mbunge hatapenda kuona
mtu ama kiongozi yeyeyo anakwamisha mradi huo kwa wananchi .
“Napenda
kuwa mkweli katika hili lengo la serikali ya chama cha
mapinduzi ni kuona wananchi wake wanaendelea
kupata maisha bora na si kwa wana CCM pekee ni
wote hata wapinzani kwani maendeleo ya umeme na mengine
hayajawalenga wana CCM ni wote …..sasa kama hivyo
ndivyo ni lazima wananchi wote kushiriki maendeleo yetu
na Yule atakayekwamisha tutashughulika nae na katika hili nitakuwa
mkali zaidi” alisema mbunge Filikunjombe
Kuwa
iwapo mtendaji wa serikali ya kijiji mwenyekiti au
diwani watabainika kuwa ni kikwazo katika uendelezaji wa
maradi huo basi ni wazi watawajibishwa wao kwanza ili
kuonyesha mfano wa wananchi kushiriki kupokea miradi.
Mbunge
huyo alisema kuwa kama mbunge atakuwa msitali wa mbele kuunga mkono
maendeleo hayo na katika kuwaonyesha mfano wananchi hao
kuwa hawakukosea katika kuchagua siku ya jumatatu atafika
eneo la mradi mapema asubuhi akiwa na vitendea kazi kwa ajili ya kuungana
na wananchi wa kata ya Lupingu katika uchimbaji wa mashimo ya nguzo za
umeme .
Katika
hatua nyingine mbunge Filikunjombe aliipongeza wizara
ya ujenzi kwa kuwaondolea kero ya miundo mbinu wakazi wa kata hiyo
ya Lupingu ambao siku zote walikuwa wakitembea zaidi ya
kilometa zaidi ya 30 kwa miguu kuelekea mjini Ludewa kupata
huduma mbali mbali kutokana na ubovu wa barabara ila kwa sasa wananchi
hao wamepatiwa barabara ya uhakika na tayari kuna usafiri wa daladala
unaotoa huduma maeneo hayo kila siku.
MAGUFULI
AVUNA WANACHAMA WAPYA 376 KATIKA VIJIJI VITATU
Mbunge wa Jimbo la Chato
ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mikono na
Wanachama wapya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walioamua kujiunga na chama hicho
mara baada ya Mbunge huyo kufanya Mkutano mkubwa wa hadhara katika kijiji cha
Nyabugela, kata ya Mganza katika Wilaya ya Chato leo.
Mbunge wa
Jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli
kihutubia mamia ya wakazi wa kata ya Mganza katika Wilaya ya Chato leo.
Wananchi wa
Kata ya Mganza wakimfurahia Mbunge wa Jimbo lao la Chato Mheshimiwa Dkt. John
Magufuli wakati akiwahutubia na kuwasisitiza wafanye kazi kwa bidii ili waweze
kujiletea Maendeleo.
Mbunge wa
Jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli
akiwapokea wanachama wapya zaidi ya 100 walioamua kujiunga na Chama cha
Mapinduzi CCM mara baada ya mbunge huyo kumaliza hotuba yake.
Wanachama
wapya wa Chama cha Mapinduzi kata ya Mganza wakila kiapo mbele ya Mbunge wao
Mheshimiwa Dkt.John Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi baada ya
kukabidhiwa kadi za uanachama hivi leo.
Waziri wa
Ujenzi ambaye pia ni mbunge wa Chato Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli amezidi
kuongeza idadi ya wanachama wapya katika Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya
mkutano wake wa siku moja kuzoa wanachama wapya 376.
Hali hiyo
imekua pigo kubwa kwa vyama vingine vya siasa kwasababu katika muda mfupi wa
mikutano ya Mbunge huyo idadi ya wanachama waliotoka katika vyama vya upinzani
imezidi kuongezeka.
Katika
mikutano hiyo iliyofanyika katika vijiji vya Nyisanzi, Kasenda na Muganza. Dkt.
Magufuli alieleza jinsi alivyotekeleza ahadi mbalimbali zilizomo kwenye za
Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kutatua kero mbalimbali za wanachi.
“Mlinichagua
kwa kura nyingi sana hapa na mimi lazima nionyeshe mfano katika kuwatumikia na
naahidi vitu vyote nilivyoahidi nimetekeleza kwa sehemu kubwa kuanzia kwenye
shule, huduma za afya, barabara, maji na umeme” alisema Dkt. Magufuli
Katika hatua
nyingine Dkt. Magufuli aliwaasa vijana kufanya kazi kwa bidii na kuacha
kudanganywa na wanasiasa uchwara.
“Nawaambia
hakuna kitu cha bure, wala hakuna mtu atakayewaletea kitu chochote kama
hamtajishughulisha, mfanye kazi muache maneno ya kukaa vijiweni” alisema Dkt
Magufuli
Akizungumza
huku akishangiliwa na umati wa watu, Dkt. Magufuli aliwataka wakazi wa Muganza
kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa za kiuchumi zinazoanza kufunguka katika
kata hiyo.
“Hapa
Muganza ndipo linajengwa lango kuu la watalii kuelekea hifadhi ya Taifa ya
Rubondo, hivyo ni bora mkajianda mapema na fursa hii, mkikaa bila kufanya kazi
fursa hizi zitawapita tu” alisema Dk. Magufuli
Aidha,
Mbunge huyo wa Chato pia alisema watanzania wanatakiwa kudumisha Amani iliyopo
isije kupotea kwani gharama yake ni kubwa.
Waziri
Magufuli alitolea mfano wa nchi za Misri, Libya na Iraq jinsi zilivyokuwa na
Amani hapo zamani lakini sasa hivi hali yake ni mbaya watu wanauana kila muda.
“Wakataeni
wanasiasa wanaohubiri siasa chafu za kuvuruga Amani, na eti kudai hadi
kieleweke vinginevyo damu itamwagika, akija mtu kama huyo mwambieni amwage damu
yake kwanza, msimkubali kwani atawapoteza” alisisitiza Dkt. Magufuli.
Katika hatua
nyingine Waziri Magufuli amewaahidi wakazi wa Muganza kuwa Serikali itamalizia
kipande cha barabara kisichozidi kilomita tatu katika kata hiyo, kwani ni ahadi
ya Mhe. Rais na tayari Wizara ya Ujenzi kwenye bajeti yake ya mwaka huu wa
fedha 2014/15 imetenga kiasi cha sh. 50.mil kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mwanzo
ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Serikali ya
CCM imeahidi na itatekeleza ahadi yake, tumejenga barabara kila kona ya nchi
hatuwezi kushindwa kumalizia kipande hichi kidogo, alisema Dkt. Magufuli .
Pia katika
mikutano hiyo waziri Magufuli alitoa michango mbalimbali katika shule na vituo
vya afya.
JESHI
LA POLISI IRINGA WALAKAMATA WATUHUMIWA WA MWANAFUNZI ALIYECHOMWA MOTO, MWILI
WAKE WAAGWA LEO
Jeshi
la Polisi mkoani iringa linawashikilia watu wanne ambao ni
walinzi wa waliokuwa wakilinda nyumba moja ya kulala wageni iliyopo kihesa
katika manispaa ya iringa kwa madai ya kumchoma moto mwanafunzi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa
Ramadhani Mungi alisema tukio hilo lilitokea Juni 24 majira ya saa tisa usiku
baada ya wasamaria wema kutoa taarifa polisi kuwa kuna mtu anatembea akiwa
anawaka moto.
Mungi alisema mara baada ya kupata taarifa hiyo Jeshi la
Polisi lilifika katika eneo hilo na kumkuta Daniel Lema
(25) akiwa ameanguka chini huku akiwa amefungwa mikono nyuma.
Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa hao waliomchoma moto kuwa
ni Mussa Nganga (28), Costa Mgayuka (38), Steven Kalole (24) na Samson
Peter (24) wote wakazi wa Kihesa waliokamatwa kabla ya kutoweka mjini iringa.
“Tulipopata taarifa tulifika eneo hilo kwa haraka na tukamkuta
ameanguka chini tulimfungua ile mikono na kumchukuza vizuri tulimkuta akipumua
kwa shida ndipo tukamkimbiza hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya
kupata matibabu.”alisema Kamanda Mungi
Alisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa baa moja inayoitwa In box bar
inayomilikiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Frederick Mwakalebela akipata
kinywaji huku akiangalia michuano ya mpira wa miguu (kombe la dunia) ambayo
inaendelea nchini brazili.
“Mwanafunzi alikuwa anaangalia michuano hiyo ya mpira wa miguu kwenye
baa hiyo na baada ya mpira huo kuisha aliondoka na kuelekea nyumbani kwake Kihesa
kabla ya kufika nyumbani eneo hilo kuna nyumba ya kulala wageni iitwayo Glory
lodge ambapo pembeni yake kuna grocery moja iitwayo Glory grocery
akaingia hapo akifikiri ipo wazi ili aendeleze kinywaji,” alisema.
Alisema
wakati akigonga mlinzi wa nyumba ya kulala wageni Glory lodge ambae ni
mmasai aitwaye Mussa Nganga alimuona na kumuita ndipo kijana akakimbia na baada
ya kukimbia alimfukuza na kuwaita wenzake watatu na kumfanyia kitendo kama
hicho.”alisema Mungi .
Baada ya kufikishwa Hospitali ya
Rufaa ya Iringa, Lema aliendelea na matibabu yake mpaka alipokutwa na mauti jumatatu
majira ya saa nane mchana.
Mwili wa Daniel Anael Lema,
aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya sheria katika Chuo Kikuu
Kishiriki cha Mt. Augustino, Tawi la Iringa (Ruaha University College - RUCO)
umeagwa jana na kusafirishwa kuelekea mkoani kwao kilimanjaro kwa mazishi.
Wanafunzi
kadhaa wa chuo hicho na baadhi ya wananchi wa manispaa ya Iringa walioguswa na
tukio hilo walijitokeza katika hospitali ya mkoa wa Iringa ambako shughuli ya
kuuga mwili huo ilifanyika.
WANNE WAFARIKI DUNIA
KATIKA AJALI YA NDEGE NAIROBI
Watu wanne wamefariki dunia asubuhi ya leo na
wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya ndege ya mizigo iliyokuwa ikielekea mji mkuu
wa Somalia, Mogadishu kugonga jengo la kibishara katika eneo la Embakasi, baada
ya kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Joseph Ngisa Mkuu wa Upelelezi katika
Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) amesema kuwa, uchunguzi wa
mwanzo umeonesha kuwa ndege hiyo ilikuwa inapaa katika masafa ya chini baada ya
kutoka uwanjani na kwamba iligonga mlingoti wa umeme kabla ya kuanguka.
Waliofariki dunia kwenye ajali hiyo ni
watumishi wanne waliokuwa ndani ya ndege hiyo ya mizigo aina ya Fokker 50.
Maafisa wa Kenya wamesema kuwa, uchunguzi
bado unaendelea ili kubaini chanzo kikuu cha ajali hiyo.
ISRAEL YASAIDIA
NIGERIA KUWATAFUTA WASICHANA
Kikosi cha Israel cha
kukabiliana na ugaidi kinatarajiwa kujiunga na juhudi za kuwatafuta zaidi ya
wasichana 200 waliotekwa nyara nchini Nigeria na wanamgambo wa kundi la Boko Haram.
Kundi hilo litajiunga na wataalamu wa
Marekani,Uingereza na ufaransa ambao tayari wako nchini Nigeria.
Rais Goodluck Jonathan amesema kuwa kujiunga
kwa Israel katika operesheni hiyo ni wazi kwamba dunia nzima inaunga mkono
usakaji wa wasichana hao.
Mwandishi wa BBC nchini Nigeria amesema kuwa
uwepo wa wataalam wa Israel katika oparesheni hiyo huenda kukazua hisia za
kisiasa nchini Nigeria ambapo wasiwasi kati ya wakristo wanaoshi kusini mwa
taifa hilo na waislamu wanaoishi kazkazini huzua ghasia.
Awali Gavana wa jimbo la Borno Kaskazini
Mashariki mwa taifa hilo, eneo ambalo wasichana hao walitekwanyara alisema kuwa
ana habari kuhusu kule walipo wasichana hao.
NICOLAS SARKOZY
AFANYIWA UCHUNGUZI
Rais wa zamani wa Ufaransa ,
Nicolas Sarkozy, amefikishwa mahakamani mjini Paris, kwa tuhuma za kutumia
nafasi yake vibaya miongoni mwa tuhuma nyenginezo kuhusiana na makosa makubwa
ya uchaguzi.
Sarkozy anajipata tena matatani tangu
kupoteza kinga ya kushtakiwa mda mfupi baada ya kupoteza kiti cha urais kwa
muhula wa pili , kilichonyakuliwa na rais wa sasa Francois Hollande hapo 2012.
Sarkozy anakana kuwa alipata ufadhili kinyume
cha sheria katika uchaguzi huo.
Awali alihojiwa kutokana na tuhuma za kufanya
ushawishi kuhusu kesi inayochunguzwa kupata ufadhili wa fedha za kampeni
kinyume cha sheria , ikiwemo kupokea fedha kutoka kiongozi wa zamani marehemu
Muamar Ghadafi.
Mwanasheria wa Bwana Sarkozy, alihojiwa
Jumatatu kuhusu tuhuma za kutafuta taarifa za ndani kuhusu kesi inayomkabili
kiongozi huyo wa zamani.
Hali ya sasa hivi inaonekana pigo kuu kwa
Bwana Sarkozy.
Wachunguzi wanajaribu kutafuta iwapo Bwana
Sarkozy, mwenye umri wa miaka 59, ambaye alikuwa rais wa Ufaransa kutoka mwaka
2007 hadi 2012, aliahidi kumpa wadhifa mkubwa jaji wa Monaco, Gilbert Azibert,
ikiwa ni shukrani ya kupatiwa taarifa kuhusu uchunguzi unaofanyika dhidi kuhusu
fedha aliyoitumia katika kampeni ya uchaguzi.
NAFASI YA UFARANSA
KWENYE MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA
Rais Paul Kagame wa Rwanda kwa mara nyingine
tena ameinyooshea kidole cha lawama serikali ya Ufaransa kutokana na kile
alichosema ni nafasi ya Paris kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika
nchi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana,
Rais Kagame alisema Ufaransa inapaswa kukiri makosa yake na kuwaomba radhi
Wanyarwanda kutokana na mchango wake kwenye tukio hilo la kuhuzunisha
lililosababisha mamia ya maelfu ya watu kuuawa.
Matamshi ya kiongozi huyo yametolewa baada ya
kufeli mazungumzo kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent
Fabius Mwezi Mei mwaka huu. Rais Kagame amewaambia wanahabari wa ndani na nje
ya Rwanda kwamba, mazungumzo pekee hayawezi kutatua hali ya mambo.
“Kama
mazungumzo yangekuwa na uwezo wa kutatua tofauti zilizoko nadhani tungekuwa
tumefikia maelewano kitambo.
Muhimu
ni kwa wenzetu kukiri walifanya makosa yao na kuomba radhi” amesema kiongozi
huyo. Hali ya kunyooshena kidole cha lawama kati ya Rwanda na Ufaransa kuhusu
mauaji ya kimbari ya 1994 imekuwa ikiyumbisha uhusiano wa pande mbili na hali
iliwahi kuwa mbaya zaidi mwaka 2006 baada ya nchi hizo mbili kukata kabisa
uhusiano wa kidiplomasia na kufunga balozi zao katika miji ya Kigali na Paris.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, mauaji ya
Kimbari ya Rwanda yalianza Aprili 6 mwaka 1994 baada ya kuuawa rais wa wakati
huo wa nchi hiyo, Juvenile Habyarimana, kufuatia kutunguliwa ndege iliyokuwa
imembeba karibu na uwanja wa ndege wa Kigali.
Rais
Habyarimana alikuwa anatoka katika kabila la Wahutu na kuuawa kwake
kulisababisha Wahutu wenye misimamo mikali kuanzisha mauaji dhidi ya Watutsi.
Mauaji
hayo yaliyoendelea kwa takriban siku 100 yalisababisha kuuawa zaidi ya watu laki
8; wengi wao wakiwa ni wa kabila la Watutsi.
Serikali ya Rwanda imekuwa ikishikilia kwamba,
Ufaransa ilihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo ya kimbari ambayo
hadi leo yanaendelea kuwashangaza wengi duniani.