SERIKALI YA
MAPINDUZI YA ZANZIBAR IMEKABIDHI RASMI HATI YA UMILIKI WA MATUMIZI YA MSIKITI
MUHAMMAD (SAW) WA MWANAKWEREKWE
Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imekabidhi rasmi hati ya umiliki wa matumizi ya Msikiti
Muhammad { SAW } uliopo nyuma ya Tawi la Benki ya Kiislamu ya Watu wa Zanzibar
{PBZ } uliopo Mwanakwerekwe kwa waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa huo ili
waendelee kuutumia katika Ibada zao mbali mbali za kila siku.
Msikiti huo
ulikuwa umefungwa kutumika kwa suala lolote la ibada kwa karibu miaka 14 sasa
tokea miaka ya 2000 baada ya kutokea hitilafu ya umiliki wa msikiti huo baina
ya waumini wa dini hiyo waliokuwa wakiutumia kwa ibada zao.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi hati hiyo kwa waumini hao
kupitia kwa Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Sheikh Abdulla
Talib na Baadaye Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Kabi ambapo amesema
waislamu wasingependa kuona msikiti huo unaharibiwa bila ya kutumika.
Balozi Seif
alisema imesikitisha kuona baadhi ya watu walikuwa wakifanya uchafu ndani ya
msikiti huo kwa muda mrefu wakati taratibu na sheria za kiislamu kamwe
haziruhusu hata kuingia na viatu ndani ya nyumba hiyo ya ibada.
Alieleza kwamba
Serikali ilifikia uwamuzi wa kuukabidhi msikiti huo kwa waumini wa eneo hilo
kufuatia vikao mbali mbali ikiwemo mahkama ya rufaa Tanzania iliyoamua kufuta
amri zote zilizohusika na msikiti huo.
“ Vikao mbali
mbali vilivyohusu suala la msikiti huo vilifikia uamuzi wa msikiti huo kutumiwa
tena na waumini kutekeleza ibada zao za kila siku “. Alisema Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa wa
Mwanakwerekwe mmoja wa Wazee wa Mtaa huo Sheikh Mwinshehe Othman ameihakikishia
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu
wataisimamia katika masuala ya ibada na si vyenginevyo.
Hata hivyo
Sheikh Mwinshere aliiomba Serikali kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
kuiangalia barabara ya kuingia kwenye msikiti huo kutokea bara bara kuu ya
mwanakwerekwe ambayo haipitiki kutokana na uchafuzi wa mazingira.
Alisema ni
vyema katika kuunga mkono nguvu za Waumini hao katika kuurejeshea hadhi yake
msikiti huo Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi au Baraza la
Manispaa likaweka nguvu zake katika kuifanyia marekebisho bara bara hiyo ili
kutoa fursa kwa waumini pamoja na wananchi kuitumia bila ya usumbufu
wowote.
Kamisheni ya
Ardhi na Mazingira Zanzibar Tarehe 16 Agosti mwaka 1991 ilitoa hati umiliki wa
ardhi ya eneo hilo kutumika kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti, Chuo pamoja na
Kituo cha Afya yenye kumbu kumbu namba MU/21 – Kiwanja D6 kikiwa na ukubwa wa
Square Metre Mia 330.
CHAPISHO LA TATU LA TAARIFA ZA MSINGI ZA
KIDEMOGRAFIA,KIJAMII NA KIUCHUMI KUZINDULIWA MEI 25, 2014
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Chapisho la Tatu la Taarifa za msingi za
Kidemografia,kijamii na kiuchumi linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012 katika ngazi ya Taifa.
Hayo
yamesemwa na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Hajjat Amina
Mrisho Said wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam
ambapo uzinduzi huo utafanyika Mei 25, mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere uliopo Dar es salaam.
Hajjat Amina
alisema kwa kifupi chapisho hilo, linatoa viashiria mbalimbali ambavyo ni
pamoja na ongezeko la idadi ya watu,mgawanyo wa watu kwa umri na jinsi,muundo
wa kaya,hali ya ndoa,hali ya ulemavu,idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi
na wale wenye vyeti vya kuzaliwa na wasionavyo.
Alivitaja
viashiria vingine ni vizazi na vifo,uhai wa wazazi,kujua kusoma na
kuandika,shughuli zaki uchumi,hali ya makazi,mifuko ya hifadhi ya jamii na
umiliki wa vifaa na huduma katika makazi.
Akifafanua zaidi kuhusu siku hiyo Hajjat Amina amesema watu wapatao 500
wanatarajiwa kushiriki katika uzinduzi huo wakiwemo viongozi wa ngazi za juu
Serikalini,Mabalozi na Wadau wa maendeleo.
Hajjat Amina
aliongeza kuwaViongozi wengine watakaoshiriki ni wa Dini,vyama vya Siasa na
Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Pamoja na wadau wa Takwimu
nchini.
Chapisho la
Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia,kijamii na kiuchumi linalotokana na
Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 ni mwendelezo wa machapisho mbalimbali
yanayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar kama ilivyoainishwa kwenye kalenda ya machapisho ya Sensa
ya watu na makazi ya mwaka 2012.
KAMPUNI TANO ZINAWANIA LESENI ZA GESI NA MAFUTA TANZANIA
Kampuni tano zimepanda dau la
kutaka kununua leseni za kutafuta mafuta na gesi katika himaya ya Tanzania.
Hata hivyo idadi hiyo ni ndogo
zaidi kuliko vitalu vinane vilivyokuwa vikinadiwa katika duru hii, TPDC
imeeleza.
Tanzania, ambayo imegundua kiasi
kikubwa cha gesi ya asili katika mikoa ya kusini, ilitangaza vitalu saba vya
maji marefu baharini na kimoja katika Ziwa Tanganyika.
Kampuni ya CNOOC Ltd na Gazprom inayoendeshwa na
serikali ya Urusi ni miongoni mwa makampuni makubwa ya kigeni yaliyowasilisha
maombi yao katika mzunguko huo wa nne.
Miamba mingine ya nishati Statoil
na ExxonMobil, ambayo imegundua kiasi kikubwa cha gesi Tanzania, iliwasilisha
maombi ya pamoja kupata kitalu kimoja.
“Mchakato wa kutathmini utaanza
mara moja na tutatangaza washindi wa mnada haraka iwezekanavyo kadri muundo wa
ushughulikiaji wa leseni unavyoruhusu,” Yona Killagane, mkurugenzi mtendaji wa
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) aliieleza Reuters.
Killagane hakusema lini washindi
watatangazwa. Muda wa mwisho kuwasilisha maombi ilikuwa Mei 15.
ATC ANGANI KUNG’ARA
SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATC) lipo karibu
kuanza
kung’ara hewani baada ya mwekezaji kutoka Oman
kuwa tayari kuwekeza kwenye shirika hilo na sasa
anasubiri serikali kukamilisha taratibu zake.
Miongoni mwa taratibu zinazosubiriwa ni kwa serikali
kulipa madeni makubwa ambayo ATC ilikuwa inadaiwa
ili kuweka mizania sawa ya vitabu vya hesabu za fedha.
Mwenyekiti na Rais wa Kampuni za
Al Hayat
Development and Investment LLC ya Oman, Sheikh
Salim Bin Abdullah Al Harthy, alisema wana dhamira ya
dhati ya kuwekeza hapa nchini na hasa katika ATC.
“Tunatarajia kuwekeza kwenye maeneo tofauti katika
sekta za mafuta na uendelezaji wa maeneo ya fukwe,
lakini lengo letu kuu ni kuwekeza ATC,” alisema Sheikh
Salim na kuwa awamu ya kwanza watatumia sh, bilioni
160.
“Mpango wetu ni kujenga kituo
cha mafunzo ya masuala
ya ndege, ofisi nzuri kwa ajili ya ATC, kununua ndege
na kufanya shughuli nyingine za maendeleo. Tunatarajia
kufanya haya katika kipindi kifupi kijacho," alisema.
Alifafanua kuwa kuna wakati
Kampuni ya Al Hayat
ilikaa kimya kuhusu uwekezaji huo na kuwa ilifanya
hivyo ili kutoa nafasi kwa serikali kukamilisha taratibu
zake ikiwemo kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya
kampuni hiyo na ATC.
Alisema watendaji wa kampuni ya
Al Hayat wamekuwa
wakitembelea Tanzania mara kwa mara ili kufuatilia
suala zima katika uwekezaji kwenye ATC.
Sheikh Salim alisema ni kutokana na hali hiyo ndiyo
maana hata ule mpango wa kununua ndege aina ya
Bombadier, Air Bus na Embraer ulisimama kidogo kwa
kuwa mkataba rasmi wa uwekezaji bado haujafikiwa na
kutiwa saini.
Alisema safari hii wamekuja tena
kuitikia wito wa ATC ili
kuendeleza makubaliano yaliyofikiwa na kuwa taratibu
zikikamilika watatia saini mkataba na kuanza uwekezaji.
Sheikh Salim alisema suala hili limechukua muda
mrefu kutokana na taratibu husika zinazohusu pande
zote, lakini anasisitiza azma ya kuwekeza iko pale pale
kwa kuwa linahusisha mambo mbalimbali ikiwemo ya
kisheria.
Hata hivyo, anasema kuna
uwezekano mkubwa ndani
ya miezi sita tangu sasa kila kitu kitakuwa kimekamilika
na ATC itarudi kung’ara angani kwa kuwa serikali
inatoa ushirikiano mkubwa na wa kutosha.
Kuhusu utoaji wa huduma, Sheikh
Salim anasema
lengo ni kuhakikisha inafika katika mikoa mingi kadri
iwezekanavyo na nchi jirani, na kufanya safari za mbali
katika nchi kama Uingereza na India.
Baada ya kukaribishwa na Sultani
Qaboos kufanya
ziara Oman, Rais Jakaya Kikwete alikutana na
wafanyabiashara wan chi hiyo na kuwakaribisha kuja
kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali.
Hivyo uwekezaji wa Al Hayat umetokana na jitihaza
zilizofanywa na Rais Kikwete katika ziara yake nchini
humo.
Kwa sasa ATC inafanya safari
zake katika mikoa ya
Mtwara, Mwanza, Tabora, Kigoma, Dar es Salaam,
Mbeya na katika nchi za Burundi na Comoro.
Hivi
karibuni itaanzisha safari za Zanzibar na Kilimanjaro.
MAGAIDI WA BOKO
HARAM WAUA WATU 30 NIGERIA
Magaidi wa kundi la Boko Haram huko Nigeria
wametekeleza jinai mpya ambapo wamewaua watu wapatao 30 kaskazini
mashariki mwa nchi hiyo.
Duru zinaarifu kuwa, Jumatatu magaidi wa Boko
Haram walivamia kijiji cha Shawa na kuwaua watu 10 na kisha jana Jumanne
wakavamia kijiji cha Alagamo na kuwaua watu 20.
Vijiji hivyo viwili viko karibu
na eneo la Chibok ambapo magaidi hao hao wa Boko Haram waliwateka nyara
wasichana wa shule wasiopungua 200.
Wakaazi wa vijiji hivyo wanasema wanagambo
wa Boko Haram pia wameteketeza moto nyumba zao. Hayo yanajiri wakati ambapo
jana watu zaidi ya 118 walipoteza maisha kufuatia hujuma ya Boko Haram katika
mji wa Jos katikati mwa Nigeria.
Wakati huo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
imelaani vikali hujuma hiyo ya Jumanne nchini Nigeria.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bi.
Marzieh Afkham ameelezea kufungamna Iran na familia za walipoteza maisha katika
hujuma hiyo ya kigaidi.
Amesisitiza kuwa Iran inapinga kila aina ya
misimamo mikali iliyo dhidi ya ubinaadamu na ametoa wito kwa kurejeshwa amani,
usalama na utulivu Nigeria.
Kwingineko, Balozi wa Nigeria nchini
Iran ameishukuru serikali na watu wa Iran kwa uungaji mkono wake wa
juhudi za kuwaokoa wasichana wa shule waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram.
Al Haj Tukuru Mani ameyasema hayo Jumatano
mjini Tehran katika kikao kilichokuwa na anuwani ya 'Mshikiamano dhidi ya
ugaidi na misimamo mikali'.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Iran na baadhi ya maafisa wa
wizara ya mambo nje ya Iran.
Balozi
wa Nigeria alisema kuwa kikao hicho ni moja ya nembo za uungaji mkono Iran kwa
juhudi za kuwaokoa wasichana wa shule waliotekwa nyara Nigeria.
Boko
Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana
na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi
hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za
kidini na kikabila nchini humo.
Aidha
kundi hilo limetoa kisingizio kwa nchi za Magharibi kutuma wanajeshi na maafisa
wa kijasusi nchini Nigeria.
SOMALIA INAKIUKA HAKI ZA WAFUNGWA - HRW
Shirika la kutetea haki za
binadamu Human rights watch limeishutumu serikali ya Somalia kwa kuwanyima
wafungwa haki za uakilishi wa wakili na kuwashitaki raia wa kawaida chini ya
mahakama za kijeshi.
Shirika hilo limesema kuwa mamia ya raia wanahukumiwa
kwa sheria kali wasizoelewa. Human rights watch pia imesema kuwa raia wengi
wamejikuta matatani baada ya kukamatwa katika msako wa kitaifa unaofanywa na
mashirika ya kijasusi ya Somalia na mara nyingie wanazuiliwa kwa muda mrefu
bila kufunguiwa mashtaka.
Kuzuiliwa kwa muda mrefu ni tatizo ndogo sana
kwa raia hao wa Somalia ikilinganishwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi na
kutishia usalama wa nchi. Ukipatikana na hatia, hukumu ni kifo.
Licha ya kuwa mashirika ya haki za binadamu
yamekuwa yakipinga kutolewa hukumu hii, Somalia ni mojawepo ya nchi chache
Afrika ambayo bado inatoa huku hiyo.
Wasiwasi mkubwa ni kwamba, washukiwa hawapewi
fursa ya kujitetea.
Na wala mahakama hizi za kijeshi hazihitaji ushahidi mwingi
kuamua kuwa una hatia.
Human rights Watch imetaja katika ripoti yao
kisa kimoja ambapo zaidi ya kesi 24 zilisikilizwa na kuamuliwa kwa chini ya
siku 4.
IRAN NA MAULAMAA WA KISHIA WASISITIZA UDHARURA WA KUKABILIANA NA BOKO
HARAM
Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia
masuala ya wanawake na familia amemuandikia barua Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa na kulaani hatua ya kutekwa nyara wasichana wa shule nchini Nigeria na
kundi la Boko Haram.
Katika
barua yake hiyo kwa Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka Naibu Katibu Mkuu wa UN
anayeshughulikia masuala ya wanawake, Shahindokht Molaverdi sambamba na
kukumbusha pendekezo la Rais wa Iran kwa ajili ya kukabiliana na machafuko na
kufurutu ada (WAVE).
Amesisitiza ulazima wa ulimwengu kukabiliana
na vitendo kama hivyo visivyo vya kibinadamu vinavyotekelezwa kwa malengo ya
kisiasa ili kuuchafulia jina Uislamu na kuwafanya watu waogope dini hii.
Barua
hiyo pia imetumwa kwa Waziri wa Masuala ya Wanawake wa Nigeria Zainab Bana,
Sekretarieti ya Mabunge ya Kiislamu, jumuiya za OIC pamoja na NAM.
Boko Haram ni
kundi la wanamgambo wenye misimamo mikali nchini Nigeria na kutokana na
kuafuata itikadi potofu wanazodai eti ni za Kiislamu, wanataka shule zote
zifungwe na kulazimisha kutumika sharia ya Kiislamu katika majimbo yote 36 ya
nchi hiyo.
Boko Haram kilugha inaamanisha, kitabu na
elimu ya Kimagharibi ni haramu, na kundi hilo linaamini kuwa elimu ya
Kimagharibu inapaswa kupigwa marufuku nchini humo.
Kundi la Boko
Haram ambalo hadi sasa limefanya vitendo vingi ya kigaidi nchini Nigeria, hivi
karibuni liliwateka nyara wasichana wa shule zaidi ya 250 katika kijiji kimoja
kilichoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kiongozi wa kundi
hilo alijitokeza na kudai kuwa, wasichana hao hawapaswi kwenda shule, wanapaswa
kuolewa na kwamba Boko Haram wanakusudia kuwauza kama watumwa katika nchi
jirani.
HAFTAR ATAKA SERIKALI YA WAKATI WA MGOGORO IUNDWE LIBYA.
Jenerali mstaafu wa Libya, Khalifa Haftar
aliyeanzisha vita dhidi ya makundi yenye silaha na kupinga serikali, ametaka
mahakama iteue serikali ya wakati wa mgogoro itakayosimamia uchaguzi mpya
nchini humo.
Haftar pia ameituhumu serikali ya mpito ya
Libya kuwa inaunga mkono ugaidi na kusema kuwa mapigano dhidi ya wanamgambo
wenye silaha yataendelea.
Hayo yanajiri huku spika wa Bunge la Libya
akiamuru kukamatwa wanajeshi walioasi na kushiriki katika mauaji ya umati ya
raia katika mji wa Benghazi.
Nuri Abusahmin ambaye pia ni kamanda wa
vikosi vyote vya ulinzi vya Libya amesema, serikali inafanya jitihada za kuzuia
mapigano zaidi kati ya makundi yenye silaha nchini humo.
Siku ya Ijumaa Jenerali mstaafu Khalifa
Haftar alitumia vikosi vya jeshi na helikopta kushambulia makundi ya wanamgambo
katika mji wa Benghazi bila ruhusa ya serikali.
Hii ni katika hali ambayo hadi
sasa wanajeshi kadhaa wa Libya wameasi jeshi na kuungana naye.