LEO NI ALKHAMISI TAREHE 7 SHAABAN MWAKA 1435
HIJIRIA, INAYOSADIFIANA NA TAREHE 5 JUNI MWAKA 2014 MILADIA.
Siku kama ya leo
miaka 51 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia sawa
na tarehe 5 Juni 1963 Milaadia, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano
makubwa dhidi ya utawala wa Shah, baada ya kusikia habari ya kutiwa mbaroni
Imam Khomeini MA.
Imam alitiwa mbaroni na vibaraka wa utawala wa Shah siku
kadhaa nyuma kufuatia hotuba yake ya kihistoria aliyoitoa katika mji wa Qum,
ambayo ilifichua njama mbalimbali za utawala wa Shah dhidi ya taifa la Iran.
Ni wazi kuwa mapambano ya umwagaji damu na ya
kihistoria ya tarehe 15 Khordad, yalikuwa nukta ya kuanza mapinduzi ya wananchi
wa Iran dhidi ya utawala wa Shah na kufungua njia ya mustakbali wa kisiasa na
kijamii nchini.
@@@
Siku kama ya leo
miaka 42 iliyopita, sawa na tarehe 5 Juni 1972, lilifanyika kongamano la kwanza
la mazingira huko Stockholm nchini Sweden. Kongamano hilo liliwashirikisha
wawakilishi 1300 kutoka nchi 113 duniani likiwa na kauli mbiu isemayo 'Kuna
Ardhi Moja tu'. Miongoni mwa malengo makuu ya kongamano hilo yalikuwa ni
kuwekwa mikakati ya kujenga makaazi ya raia kwa kuzingatia ulindaji mazingira,
kuainisha na kudhibiti mada haribifu kwa mazingira na kuhifadhi mazingira kwa
ajili ya vizazi vya baadaye.
@@@
Siku kama ya leo
miaka 47 iliyopita muwafaka na tarehe 5 Juni 1967, vilianza vita vikubwa vya
tatu kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Kiarabu. Katika siku kama
ya leo kikosi cha anga cha utawala ghasibu wa Israel kilifanya shambulizi la
kushtukiza na kuvuka mipaka ya nchi tatu za Misri, Syria na Jordan na kufanya
uharibifu mkubwa. Baada ya shambulizi hilo, vikosi vya nchi kavu vya Israel
vikiwa na silaha za kisasa na uungaji mkono wa Marekani na Uingereza,
vilifanikiwa kuyashinda majeshi ya Misri, Syria na Jordan katika kipindi cha
siku sita tu.
WAPINZANI NCHINI TANZANIA WAZIDI KUISAKAMA
SERIKALI
Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimezidi
kuisakama Serikali vikisema kuwa hivi sasa kila mtanzania ana deni la Shilingi
600,000 kutokana na fedha zilizokopwa kuendeshea warsha, semina, safari,
mafunzo na matengenezo ya magari.
Vyombo vya habari nchini Tanzania vimemnukuu
Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia akiwasilisha taarifa ya kambi ya Upinzani
bungeni na kusema kuwa, deni la taifa limeongezeka kwa Shilingi trilioni 8.2
kwa kipindi cha miezi saba tu na kwamba ukiligawanya deni hilo kwa idadi ya
Watanzania milioni 45, kila mwananchi atakuwa anadaiwa Shilingi laki sita
(600,000).
Vyombo hivyo vimeongeza kuwa, karibu fedha
zote zilizotengwa na Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, zitatumika
katika kulipia Deni la Taifa. Vimesema, kati ya Shilingi trilioni 5.8 za bajeti
ya Wizara ya Fedha mwaka 2014/15, Shilingi trilioni 4.3 zimetengwa kwa ajili ya
kulipia Deni la Taifa.
Wapinzani hao pia wamesema, ingawa serikali
ya Tanzania inasema kuwa deni hilo linavumilika, lakini linaonekana kuwaelimia
Watanzania kwani hata mapato ya ndani yamezidiwa na matumizi ya kawaida hivyo
kuifanya Serikali kukopa hata kwa ajili ya warsha, semina, safari, mafunzo na
matengenezo ya magari.
TANZANIA YAWA YA KWANZA AFRIKA MASHARIKI KATIKA
USAFIRI WA MABASI YAENDAYO KASI---PINDA.
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuingia kwenye ubia na sekta binafsi katika mradi mkubwa wa
usafirishaji abiria.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Juni 3,
2014) wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano yenye lengo la kuutangaza mradi
wa mabasi yaendayo kasi kwenye ukumbi wa Mlimani City. Mkutano huo wa siku
mbili, utamalizika kesho (Jumatano, Juni 4, 2014).
Waziri Mkuu amesema kutèkelezwa kwa mradi huo
kutatoa fursa za ubunifu utakaowezesha kupatikana kwa suluhisho la usafiri
mijini na hasa kwenye miji inakua kwa kasi barani Afrika.
"Mbali ya kutoa huduma za hali ya juu, za
haraka na ambazo siyo ghali kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, nia ya Serikali
ni kuona mfumo mpya wa matumizi ya kadi kwenye mpango huu wa usafiri unatumika
ipasavyo," alisema.
Alisema ni matumaini ya Serikali kwamba wadau
kutoka sekta binafsi ambao ni wazawa na wa kutoka nje ya nchi watashiriki
kwenye mradi huu ili uweze kuboresha matumizi ya kadi ambayo mtu hatatakiwa
kulipia fedha taslimu akiwa ndani ya basi bali kutumia kadi anayoilipia kabla
ya kuingia ndani ya basi husika.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali iliamua kuanzisha mradi huo
ili kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara za Jiji la Dar es Salaam.
"Hii ni awamu ya kwanza ambayo inakaribia
kukamilika na inaanzia Kimara hadi Kivukoni na itakuwa na matawi mawili ya
Morocco na Karikoo. Mradi wote una awamu sita za ujenzi kuelekea maeneo tofauti
ya Jiji," alisema.
Mbali na mradi huo wa mabasi yaendayo kasi,
Serikali inaangalia uwezekano wa kutumia usafiri wa majini kwa kutumia boti
kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa
magari jijini Dar es Salaam.
“Vilevile tutaimarisha usafiri wa reli kama njia
nyingie ya kupunguza tatizo hili. Dk. Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi) ameanza na
sote tumeona ni jambo linalowezekana. Cha msingi ni kuimarisha tu usafiri huu,” aliongeza
Waziri Mkuu.
Akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia alisema Serikali
imedhamiria kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa.
Pia alitumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya Dunia
ambayo alisema imetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya
kufadhili mradi huo.
Mkutano huo unawashirikisha wadau mbalimbali
wakiwemo wa ndani na wa nje wanaotarajiwa kutoa huduma za mabasi makubwa na
madogo, utoaji tiketi, ulinzi, usafi na huduma za maduka.
POLISI IRINGA YASAMBARATISHA MTANDAO
WA WAVUTA BANDI
Jeshi la polisi mkoa wa Iringa limefanikiwa
kuusambaratisha mtandao wa bangi katika eneo la Isakalilo
mjini Iringa baada ya kufanikiwa kukamata mzigo wa bangi
uliokuwa ukiandaliwa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi amesema kuwa
tukio hilo limetokea juzi baada ya jeshi la polisi kubaini
kuwepo kwa mtandao huo .
Alisema kuwa wakati polisi wakijiandaa kuzingira nyumba hiyo
ambayo haijaisha (Pagale) mmoja kati ya vijana waliokuwa
wakiiandaa bangi hiyo aliwaona polisi hao hivyo kulazimika
kuruka dirishani na kutelekeza bangi hiyo yenye uzito wa kg 10.
Hata hivyo alisema kuwa hakuna aliyekamatwa japo polisi
wanaendelea na msako zaidi na kuwataka wananchi kutoa
ushirikiano kwa jeshi hilo la polisi.
WANAWAKE WAENDELEA KUTUPA WATOTO
WACHANGA MBEYA.
WIMBI la wanawake mkoani Mbeya kujifungua watoto na kisha kuwatupa na
wengine kutoa mimba limezidi kushika kasi na kukithiri baada ya vitendo hivyo
kuripotiwa na vichanga kuokotwa kwenye mashimo na mitoni.
Kukithiri kwa vitendo ni baada ya jana Wananchi wa Mtaa wa Mwambenja
kata ya Iganzo jijini Mbeya kugundua kutupwa kwa mtoto anayesemekana kuwa na
umri usiozidi siku moja jinsia ya kike katika shimo la choo kisichotumika.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Mtaa huo, aliyefahamika kwa jina la Lukasi
Mwakalonge, alisema alipewa taarifa na wananchi wake mchana na kuambiwa kuna
katoto kametupwa shimoni na bado ni kazima hali iliyomlazimu kutoa taarifa
katika Jeshi la Polisi.
Alisema baada ya kufika eneo la tukio na kugundua kuwa mtoto bado yuko
hai wakaamua kumtoa ndani ya shimo huku wakisubiri jeshi la polisi kwa ajili ya
hatua zaidi lakini akawa amepoteza maisha muda mfupi baada ya kutolewa ndani ya
shimo.
Hata hivyo jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa
marehemu, vitendo hivyo vya wanawake kutupa watoto kabla na baada ya kujifungia
bado vinazidi kutokea hapa nchini ingawa hakuna takwimu sahihi za wanawake
waliopatikana na hatia kwa makosa kama hayo.
MABAKI YA MKONGE KUZALISHA SUKARI.
KAMPUNI
ya Katani ipo kwenye hatua za mwisho za mazungumzo kuhusu ukubwa wa kiwanda cha
kuzalisha sukari kutokana na mabaki ya mkonge, itakayotumika kwa wagonjwa
wenye kisukari.
Hayo
yamesemwa na Mkurungezi wa Maendeleo Katani Juma Shamte alipozungumza kwenye
semina ya wazi iliyofanyika kwenye viwanja vya Tangamano jinsi wakulima
watavyonufaika na mkonge.
Alisema
kuwa kwasasa wapo kwenye mazungumzo ya mwisho na kampuni itakayojenga kiwanda
hicho nchini kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.
Shamte
alisema kiwanda hicho kitakapo kamilika ujenzi wake na kuanza kazi kitawezesha
kupungua uhaba wa sukari nchini na nyingine kuuzwa kwenye masoko ya kimataifa.
Kwa
upande wa mahitaji kwenye soko la dunia, Shamte alisema uhitaji wa bidhaa za
mkonge umezidi kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 15 ya bei ukilinganisha na
mwaka 2000 ambapo bei ilikuwa chini.
Hata
hivyo aliwahimiza wakulima kulima mkonge kwa wingi ili kujiongeza kipato
maradufu kutoka na zao hilo kuwa na soko la uhakika ndani ya nchi na hata nje
ya nchi.
"Mfumo
wa masoko si wa kugawana mapato kwani zao hili linamuwezasha mkulima kupata
mapato yake mwenyewe na kampuni ya katani kazi yake ni kumuwezesha mkulima
kupata pembejeo pamoja na kumtafutia soko la uhakika la kuuza bidhaa
zake,"alisema Shamte.
G7 WAKUTANA BRUSSELS BILA URUSI
Kundi la G7 la nchi zinazoongoza kwa viwanda
duniani limetishia kuiwekea Russia vikwazo zaidi kutokana na mgogoro wa
Ukraine.
Taarifa ya kundi hilo linalozijumuisha nchi za
Marekani, Canada, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Japan na Italia imeitaka
Moscow kuacha kile ilichokitaja kuwa ni 'kuvuruga hali ya ndani ya Ukraine' au
wataiwekea vikwazo zaidi.
Wakati huo huo Rais Barack Obama wa Marekani
imeituhumu Moscow kuwa inatumia 'mbinu giza' za karne ya 20 nchini Ukraine, na
kuahidi kukabiliana na kile alichodai ni uingiliaji wa Russia huko mashariki
mwa Ukraine. Obama amesema hayo huko Brussels anakohudhuria mkutano wa kundi la
G7.
SYRIA YAPATA MAFANIKIO KATIKA VIUNGA VYA DAMASCUS
Vikosi vya jeshi la Syria vimepaata mafanikio
mapya katika mapambano dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na nchi za nje,
karibu na mji mkuu Damascus.
Jeshi la Syria limefanikiwa kudhibiti eneo la
kaskazini na mashariki mwa nji wa Mleha, baada ya kupambana kwa siku kadhaa na
magaidi.
Wakati huo huo vikosi vya serikali ya Syria
vimewafurusha wanamgambo wenye silaha katika maeneo ya pambizoni mwa miji ya
Homs, Daraa, Lattakia na Idlib, mafanikio yanayohesabiwa kuwa kipigo kikubwa
kwa magaidi hao wanaoungwa mkono na nchi za kigeni dhidi ya maficho yao.
Wakati huo huo mmoja wa wagombea wa uchaguzi
wa rais wa Syria amempongeza Rais Bashar al Assad kwa kushinda uchaguzi huo na
kutangaza kuwa yupo tayari kushirikiana naye. Hassan Abdullah al Nouri leo
amempongeza Rais Assad kwa kushinda katika uchaguzi huo wa Jumanne na kusema
kuwa, hatua inayofuata baada ya uchaguzi ni kushirikiana kwa lengo la kuijenga
nchi.
Bashar al Assad ameshinda uchaguzi wa rais wa
Syaria kwa kupata asilimia 88.7 ya kura za wananchi.
UN YATIWA HOFU NA
KUENDELEA MACHAFUKO S/KUSINI
Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
amelaani kuendelea umwagaji damu nchini Sudan Kusini kutokana na kutoheshimiwa
makubaliano ya usitishaji vita na kuzitaka pande hasimu za mgogoro wa nchi hiyo
kuacha operesheni zote za kijeshi na kushikamana na ahadi za huko nyuma.
Ban
amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Rais Salva Kiir wa nchi
hiyo.
Aidha katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
ameelezea wasiwasi wake kutokana na kuendelea uadui ambao ni kinyume na makubaliano
ya Januari 23 ya kuacha uadui, na pia makubaliano ya Mei 9 yaliyotiwa
saini kati ya Rais Salva Kiir na makamu wa rais wa zamani wa Sudan Kusini Riek
Machar.
Mapigano nchini Sudan Kusini yamepelekea
maelfu ya watu kuuawa na zaidi ya watu milioni 1.3 kuwa wakimbizi.
Umoja wa Mataifa huko nyuma ulisema pia kuwa,
kuheshimiwa usitishaji mapigano ni muhimu ili kuboresha hali mbaya ya
kibinadamu inayoshuhudiwa katika nchi hiyo.