CUF YAFANYA UCHAGUZI WAKE WILAYA YA MJINI
Chama cha Wananchi CUF leo kimeendelea na uchaguzi wake ngazi ya
Wilaya kuwachagua viongozi mbali mbali wakiwemo Makatibu wa Wilaya, Wenyeviti
pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu Taifa.
Viongozi
wengine wanaochaguliwa ni wajumbe wa kamati tendaji pamoja na wajumbe wa
viti maalum ngazi ya Wilaya.
Akifungua
mkutano mkuu wa uchaguzi Wilaya ya Mjini unaofanyika ukumbi wa Basra Mtoni
Kidatu, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad Massoud Hamad, amesema viongozi
wote watakaochaguliwa wana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya chama hicho ngazi ya
Taifa.
Hivyo amewataka wajumbe wa mkutano huo kuwa makini katika uchaguzi huo, ili
kuwachagua viongozi watakao kuwa tayari kukitumikia chama, na kuepuka
kuwachagua viongozi kwa sababu ya kujuana.
Amesema lengo la chaguzi hizo ni kuimarisha na kujenga chama kwa kufuata
misingi ya demokrasia, na kuwasisitiza wajumbe hao kutochagua viongozi wenye
makundi, misimamo ndani ya chama, na badala yake wachague viongozi majasiri na walio
tayari kujitolea, ili kukiwezesha chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015.
Mhe. Hamad Massoud ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Ole (CUF), ametanabahisha
kuwa iwapo wajumbe wa mkutano huo watawachagua viongozi wasio kuwa na sifa,
baraza kuu la uongozi linayo mamlaka ya kutengua uamuzi huo na kuitisha chaguzi
nyengine.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, nae ameungana na wajumbe wa
mkuano huo wa CUF Wilaya ya Magharibi, kuchagua viongozi wa Wilaya watakao
kiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Uchaguzi huo unaendelea katika Wilaya za Magharibi, Kaskazini “B”, Kati na
Kusini Unguja, baada ya kukamilika kwa chaguzi hizo katika Wilaya zote nne za
Pemba na mbili za Unguja, hatua ambayo inakamilisha chaguzi hizo kwa Wilaya
zote za Zanzibar.
Mchakato wa uchaguzi huo utaendelea kesho kwa wajumbe wa mkutano mkuu Taifa
kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea kuchaguliwa katika baraza kuu la uongozi
Taifa.
TANZANIA
YAWAKAMATA WASHUKIWA 16 WA AL-SHABAAB KWA MASHAMBULIZI YA MABOMU ARUSHA
Jeshi la polisi nchini Tanzania limewakamata
washukiwa 16 wanaohusishwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya mabomu mjini Arusha ambayo yaliwaua watu
watano.
Mkurugenzi wa Upepelezi wa Jinai, Isaya
Mngulu, alisema washukiwa hao walihusishwa na kundi la kigaidi la al-Shabaab.
"Bado operesheni inaendelea kwani kuna
washukiwa wengi wanaohusishwa na mashambulizi ya mabomu yaliyotokea Arusha
ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita," Mngulu aliwaambia waandishi wa
habari.
Washukiwa hao walipelekwa mara moja kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkaazi wa Arusha ambako walisomewa mashtaka 16, likiwemo la
kujaribu kuua na kuwachochea vijana wajiunge na al-Shabaab.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 11 Juni.
POLISI YATOA TAARIFA YA
VIFO VILIVYOTOKEA MWISHONI MWA JUMA DODOMA.
Watu wawili wamepoteza maisha kutokana na ajali mbili zilizotokea
katika maeneo mawili tofauti na nyakati tofauti Mkoani Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID
MISIME – SACP ameeleza kuwa, ajali ya kwanza ilitokea tarehe 30/05/2014 majira
ya saa 18:30hrs katika kijiji cha Ipala Wilaya ya Dodoma ambapo gari lenye
namba za usajili DFP 614 Toyota Land Cruiser mali ya chuo cha Serikali za Mitaa
Hombolo likitokea chuoni kuelekea Dodoma mjini likiendeshwa na ALFRED MLIGO, MIAKA 35, MHEHE, liliacha njia na
kupinduka na kusababisha kifo chake.
Pia watu watano walipata maumivu mbalimbali na walitibiwa na
kuruhusiwa.
Mwili wa marehemu upo katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma
kusubiri taratibu nyingine.
Kamanda MISIME AMESEMA ajali ya pili imetokea majira ya saa 18:45hrs
huko katika kijiji cha SILWA barabara ya Dodoma – Morogoro ambapo gari lenye
namba za usajili T.150 CWA Toyota Granvia Station Wagon likiendeshwa na MGENI
S/O SHEMAKAME, MBONDEI, MIAKA 29 MKAZI WA MBURAHATI DSM liliacha njia na
kusababisha kifo cha GEORGE S/O TYSON, MIAKA 39, MWONGOZAJI WA FILAMU, Mkazi wa
mbezi DSM.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Gairo
ukisubiri taratibu za Polisi na wanandugu.
Pia katika ajali hiyo wanahabari wanne (4) wa Mboni show walipata
majeraha mbalimbali na kutibiwa na kuruhusiwa, ambao ni:-
1. NIXON KABUMBILE, MHAYA, MIAKA 31
2. GRACE MEENA, MCHAGA, MIAKA 28
3. NTWA KABOLE, MNYAKYUSA, MIAKA 33
4. JUSTINE BAYO, MIAKA 27, MMASAI
Uchunguzi wa awali unaonyesha ajali zote mbili zimesababishwa na
mwendokasi.
Kamanda MISIME ametoa wito kwa madereva kuepuka mwendokasi na kuwa na
udereva wa kujihami ambao unasaidia dereva kusimama bila kusababisha madhara
linapotokea jambo lolote na hata kama ajali ikitokea madhara hayawezi kuwa
makubwa kama yanavyokuwa anapokuwa kwenye mwendo wa kasi
TANAPA YATOA UFAFANUZI JUU
YA MADAI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI.
MENEJA
Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa ,Paschal Shelutete ametoa ufafanuzi
wa juu ya madai ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu tuhuma za Ufisadi
dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe.
Ufafanuzi
huo unakuja siku chache baada ya msemaji wa kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni kupitia Waziri wake kivuli wa wizara ya
Habari,Michezo,Vijana na utamaduni kudai Zitto alihusika
kinachotajwa ufisadi katika shirika la TANAPA
na NSSF.
Shelutete
amesema TANAPA linakitambua kiasi hicho kilichotajwa
na wapinzani na kwamba fedha hizo ilikuwa
ni malipo ya wasanii wa Leka
Dutigite ambao walifanya kazi ya
kuitangaza Hifadhi ya Saadan.
“Leka
Dutigite ilifika Hifadhi ya Saadan na kuitangaza kupitia kazi za sanaa...
sikumbuki ni lini lakini walifanya kazi na DvD zake zipo."Alisema
Shelutete.
“Ifahamike
si Leka Dutigite pekee, tunafanya kazi na wasanii mbalimbali kutangaza vivutio,
mbuga na hifadhi zetu,”aliongeza Shelutete .
Kwa
upande wao NSSF kupitia kwa Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma kwa
Wateja , Eunice Chiume amesema kuwa pesa walizozitoa kwa kundi hilo zilikuwa
malipo ya kutengenezea wimbo maalumu wa shirika hilo na nyingine ni za udhamini
wa onyesho lililofanyika mwaka jana mkoani Tanga.
“Kweli
mara ya kwanza tuliwalipa Sh25 milioni wasanii wa kundi hilo ili watutengenezee
wimbo na Sh56 milioni zilikuwa za udhamini wa onyesho lao, lakini kwa masharti
ya kututangaza jambo ambalo lilikuwa na mafanikio kwetu kwani tumefanikiwa
kupata wateja wapya 30,000 kutoka sekta isiyo rasmi,” alisema Chiume.
Alisisitiza
kuwa wametumia kiwango hicho cha pesa ili kujitangaza kwa kuwa hata mashirika
ya kijamii yanapaswa kufanya hivyo ili kuvutia wateja wengi zaidi
MAKASISI WALIOTEKWA NYARA
WAACHILIWA.
Kituo cha uhamiaji kati ya
mpaka wa Cameroon na Nigeria
Makasisi wawili kutoka nchini
Italy pamoja na mwanamke mmoja raia wa Canada waliotekwanyara na kundi la Boko
Haram nchini Cameroon wameachiliwa huru.
Idara ya mawasiliano nchini Cameroon imesema
watatu hao wako katika afya nzuri na wameabiri ndege inayoelekea katika mji
mkuu wa Younde.
Walipelekwa kazkazini mwa taifa hilo karibu
na mpaka na Nigeria.
Majina ya makasisi hao ni Giampaolo Martana
na Giantonio Allegri.
WAHANGA WA MAUAJI
YA BOKO HARAMU WAONGEZEKA
Idadi ya wahanga wa shambulizi la jana la
kundi la Boko Haram katika mpaka wa Nigeria na Cameroon, imeongezeka na kufikia
watu 42.
Kwa
mujibu wa habari zilizothibitishwa na maafisa usalama nchini Nigeria, watu
wasiopungua 42 waliuawa katika shambulizi hilo jipya lililofanywa na wanachama
wa kundi hilo katika vijiji vya Kanari, Wazarde na Gula katika jimbo la Borno,
la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Inaelezwa kuwa vijiji hivyo viko katika eneo
la Gamboru karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon ambapo mwanzoni mwa mwezi
uliopita kundi hilo lilifanya mauaji ya kutisha dhidi ya watu wasiopungua 300.
Mashuhuda wameeleza kuwa, watu wenye silaha
wanaosadikiwa kuwa wanachama wa Boko Haram na ambao walikuwa katika malori
yaliyokuwa yamebeba silaha na mada za miripuko walivamia vijiji hivyo na
kuviteketeza kwa moto, ambapo mbali na kuua idadi kubwa ya watu, walijeruhi
mamia ya wengine. Mashambulizi hayo yaliendelea kwa muda usiopungua masaa saba,
na cha kushangaza ni kuwa hakuna askari yeyote wa serikali aliyefika eneo hilo.
Hali
hiyo imewafanya asilimia kubwa ya Wanigeria kuamini kuwa mashambulizi hayo
yanafanyika kwa baraka za maafisa usalama wa nchi hiyo.
WAASI WA ANTI-BALAKA JAMHURI YA AFRIKA YA
KATI WAHARIBU MSIKITI
Huku machafuko yakizidi kushika kasi nchini
Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa mara nyingine tena, waasi wa Kikristo wa
Anti-Balaka wamevamia msikiti mmoja mjini Bangui na kuuharibu kabisa.
Hii ni
katika hali ambayo hivi karibuni pia kanisa moja mjini humo lilishambuliwa na
watu wenye silaha wanaosadikiwa kuwa na mafungamano na waasi hao na kufanya
mauaji dhidi ya watu wasiopungua 30 akiwemo padri wa kanisa hilo.
Kufuatia kuongezeka wimbi la vitendo vya
ukatili nchini humo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, sambamba na kutoa
tamko kuhusiana na suala hilo, limeyataka makundi yanayohusika katika vitendo
hivyo, kuweka chini silaha na kufuata mkondo wa amani nchini humo.
Katika ripoti hiyo Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa limeitaka serikali ya Rais Catherine Samba-Panza wa Jamhuri ya Afrika
ya kati, kuwachukulia hatua kali na za haraka wahusika wa vitendo hivyo.
Vile vile
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR
amelaani shambulizi hilo dhidi ya kanisa mjini Bangui, na kuyataja machafuko
hayo ya hivi karibuni kuwa ni dalili za kuzorota hali ya usalama nchini humo.
Adrian
Edwards amelaani mashambulizi dhidi ya maeneo ya ibada ambayo ndio maeneo
yaliyosalia kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi na kutaka kukomeshwa
mashambulizi hayo mara moja.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, wakazi wa mjini
Bangui, wamefanya maandamano makubwa mjini humo wakimtaka Rais Panza ajiuzulu
kutokana na kile wanachodai kuwa ni kushindwa serikali yake ya mpito kumaliza
machafuko nchini mwao.