Waumini katika kanisa moja nchini
Kenya wanakila sababu ya kumshukuru mola wao baada ya bomu iliyokuwa
imetegwa ndani ya kanisa kupatikana wakati wa ibada.
Waumini hao
wa kanisa katoliki la Kutus lililoko eneo la katikati ya nchi walitoroka
kanisani baada ya muumini mmoja kuona kifaa kilichokuwa kimefichwa
chini ya viti alipokuwa akitoa sadaka na kuwatahadharisha wenzake.
''Tulipokuwa
tukienda kutoa sadaka niliona kitu kilichokuwa kinafanana kama
kisanduku kidogo na nyaya ,nilihofu sana nikamweleza padri'' alisema
bwana Richard Kanyuiro.
Afisa mmoja wa polisi wa utawala aliyeitwa
kushuhudia alikitambua kifaa hicho kuwa ni bomu na hivyo wakawaarifu
waumi waliotorokea usalama wao.
Maafisa wa usalama kutoka Nyeri na
Embu waliitwa na kuwaondoa waumi wote karibu na kanisa hilo huku
wakiwasubiri maafisa wenye uwezo wa kuharibu mabomu kuwasili kutoka
Nairobi.
Mwenyekiti wa waumini katika eneo hilo bwana Paul Njeru,
anasema kuwa huenda kilipuzi hicho kiliwekwa mapema siku ya jumapili
katika sala ya alfajiri kwa nia ya kukilipua wakati wa misaa.
Kasisi
Njenga anayesimamia kanisa hilo anasema ilikuwa ni bahati tu na huruma
ya mwenyezi mungu kuwa kifaa hicho hakikulipuka wakati waumini wamejaa
kanisani.
''Ni mkono wa mungu tu kuwa kilipuzi hichi hakikulipuka wakati wa ibada''
Majuzi
tu Idara ya polisi nchini Kenya ilitangaza tahadhari mbali na kutaja
majina ya washukiwa 11 wa ugaidi wanaodaiwa kuwa wameingia humu nchini
kutoka somalia kwa nia ya kutekeleza mashambulizi haswa wakati huu wa
krismasi.