RPC. DAVID A. MISIME
Jeshi la
Polisi Dodoma limewatahadharisha wananchi
kutokufanya fujo wakati wa mkesha wa mwaka mpya kwa kuweka mikakati
mikali kwa watakaokaidi amri hiyo.
Akizungumza leo mjini Dodoma kwenye kipindi Cha Sunset In Dodoma kinachorushwa na kituo cha Redio Mwangaza Fm, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma David Misime amepiga marufuku uchomaji wa
matairi ya gari, upigaji baruti, risasi za moto na fataki ambazo zaweza
kusababisha madhara wakati wa mkesha wa mwaka mpya.
“ Ni
baraka zaidi kusherekea sherehe kama hizi kifamilia na sio vizuri
kuingia mwaka mpya ukiwa mahabusu, au kuamkia mahakamani, au gerezani kwani huo ni mkosi” Alisema Kamanda Misime.
Kamanda Misime aliongeza kuwa watashirikiana na wadau mbalimbali kufanya doria ili
kuhakikisha kuwa wanailinda amani na kudhibiti aina yoyote ya uhalifu
utakaojitokeza.
Aidha
Kamanda Misime amesisitiza kuwa vituo vyote vya polisi vitakuwa wazi
masaa 24 ili kuwawezesha wananchi kutoa taarifa haraka pindi wanapopata
matatizo au wanapoona dalili zozote za uvunjifu wa amani.
Katika
kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka wa 2015 Jeshi la Polisi Dodoma limetoa rai kwa wananchi kushirikiana na Jeshi
hilo katika kuzuia uhalifu kwa kutoa taarifa haraka pindi waonapo dalili
za uvunjifu wa amani.
Aidha Kamanda Misime amewatakia wananchi waishio mkoani Dodoma Heri ya mwaka mpya wa 2016.