“Unakuja
kwenye ofisi yangu na kutoa taarifa za ubadhirifu wa mtendaji wa kijiji.
Nakuuliza, je umechukua hatua zipi kama kiongozi wa kijiji kabla kuja
kwenye ofisi yangu? Unanijibu hapana, hii si sahihi,”
Hayo ni
maneno ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa, aliyoyatoa
wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata
na vijiji kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Loliondo, mwezi
Agosti mwaka huu.
Alisema
hayo kwa lengo la kufafanua dhana ya uwajibikaji kwa viongozi kama njia
muhimu ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo ya vijijini
katika wilaya yake.
Ni dhahiri kwamba viongozi wa ngazi za vijiji na kata wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji katika maeneo husika.
Kuna
nafuu kwa watendaji wa kata na vijiji, ambao ni waajiriwa wa serikali
na hupewa kazi kutokana na miongozo, lakini siyo kwa wenyeviti wa
vijiji na madiwani, wakati mwingine hata wabunge.
Akielezea
changamoto hiyo wakati wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji kupitia mradi
wa Chukua Hatua yaliyofanyika Septemba mwaka huu na shirika mdau la
CABUIPA, mwenyekiti wa kijiji cha Nyakafulu kilichopo wilaya ya Mbogwe,
mkoani Geita, Salum Said amesema:
“Baada ya
kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kijiji hiki, hakika sikufahamu vya
kutosha kuhusu majukumu yangu mapya kama kiongozi. Na hii ni changamoto
kubwa kwa wenyeviti wa vijiji karibu vyote vya wilaya yetu.”
Yeye ni mmoja kati ya wenyeviti 200 wanaopatiwa mafunzo katika mikoa ya Shinyanga, Geita na Simiyu.
Hii ni
kutokana na ukweli kwamba, katika awamu ya kwanza ya mradi wa Chukua
Hatua, nguvu kubwa iliwekwa katika kuwawezesha wananchi kuwachukulia
hatua watendaji na viongozi wabadhirifu wa mali za umma.
Wakati
wananchi wakiwezeshwa kuwasimamia viongozi wao, viongozi hawakuwa
wakiwezeshwa kutimiza majukumu yao kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi
wao. Hivyo, haja ya kutoa mafunzo kwa viongozi hao ili waweze kutimiza
majukumu yao kwa wananchi waliowachagua, ilikuwa lazima.