WATU wapatao 20 wanasemekana kufa huko Maiduguri, Jimbo la Borno nchini Nigeria baada ya bomu kulipuka msikitini jana.
Kwa
mujibu wa gazeti la Premium Times, wengi wa waliouawa wanaaminika ni
wakazi wa eneo hilo ambao walikuwa wamekusanyika katika msikitu huo
kufuatia uvumi kwamba kulikuwa na bomu lililokuwa limeachwa humo.
“Sijaona
kitu cha kipumbavu kama hiki ambapo watu waliingia katika msikiti
kuchunguza iwapo kweli kulikuwa na bomu. Kweli bomu lilikuwemo na
likalipuka na kuua watu zaidi ya 20 na wengi kujeruhiwa,” alisema ofisa
mmoja wa polisi akiongea na gazeti hilo.
Hata hivyo, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, alisema ni kawaida kwa wakazi wake kukusanyika eneo la msikiti kila asubuhi.
“Watu
hukaa eneo la msikiti kila asubuhi ambapo kwa ajili ya maongezi na
kupumzika,” alisema mkazi mmoja na kuongeza kwamba bomu hilo lilikuwa
si la kujitoa mhanga bali liliwekwa makusudi na watu fulani.
Shambulizi
la wapiganaji wa Boko Haram jana liliua watu 15 wa familia moja baada
ya mwanamke mmoja aliyekuwa na mabomu kujilipua baada ya familia hiyo
kumkaribisha nyumbani kwao wakiamini alikuwa anakimbia magaidi.