Mchezaji bora wa Afrika kwa
wachezaji wa nyumbani Mbwana Samatta amekabidhiwa sehemu ya ardhi na
serikali ya Tanzania kufuatia uhodari wake uliomwezesha kuondoka na tuzo
hiyo na kuisaidia TP Mazembe kutwaa kombe la vilabu bingwa Afrika.
Mchezaji
huyo pia alitunukiwa zawadi nyinginezo kwenye hafla iliyoandaliwa ili
kusherekea mafanikio yake katika soka yaliyoiweka Tanzania katika ramani
ya soka.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wadau wa michezo nchini
Tazania wakiwemo waziri wa michezo Nape Nnauye na Thomas Ulimwengu
ambaye ni mchezaji mwenza wa Samatta.
Amepewa kipande cha ardhi eneo la Kigamboni, Dar es Salaam na serikali kupitia wizara ya ardhi na nyumba.
Mchezaji huyo pia ameteuliwa nahodha mpya wa timu ya taifa Taifa
Stars, nafasi ambayo awali ilishikiliwa na beki Nadir Haroub
‘Cannavaro’ anayeichezea klabu ya Yanga.
Samatta, maarufu ‘Samagoal’ aliwapiku Robert Kadiaba na
Bounedjah Baghdad wa Algeria anayeichezea klabu ya Etoile du Sahel na
kutwaa tuzo hiyo.
Baada ya kupokea taji lake katika
sherehe za kuwatuza wachezaji bora Afrika, mjini Abuja, Samatta alirejea Tanzania na baadaye kualikwa na Rais wa Zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete.
Mnamo
mwaka wa 2013, serikali ya Nigeria iliwakabidhi wachezaji wake sehemu
ya ardhi mjini Abuja na pesa kwa kushinda kombe la Afcon.