Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima (kulia) akizungumza na waandishi wa
habari makao makuu ya klabu hiyo, kushoto ni afisa habari wa Yanga Jerry
Muro.
Kiungo wa kutumainiwa wa Yanga na timu ya taifa ya Rwanda amerejea
kwenye timu yake ya Yanga baada ya kutimuliwa na uongozi huo kutokana na
sababu za kinidhamu.
Jana January 17, 2016 Niyonzima ameomba radhi kwa wanachama, viongozi
na wachezaji wenzake kwa kile ambacho kilitokea miezi michache
iliyopita. Niyonzima ameshaomba radhi mbele ya waandishi wa habari na
kwa sasa anasubiri taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa Yanga kuhusu
suala kusamehewa kwake.
“Nitumie fursa hii kuwaomba radhi viongozi, wanachama, wachezaji
wenzangu pamoja na mashabiki wa Yanga kutokana na yale yote yaliyopita
nyuma. Mimi niliondoka kwenda kuichezea timu yangu ya taifa ya Rwanda
lakini nilichelewa kurejea kwenye klabu yangu na hapo ndipo matatizo
yalianza”, amesema Niyonzima.
“Kiukweli nilikosea kwasababu sikutoa taarifa kwa timu yangu na
ikachukua uamuzi wa kunifukuza kwenye timu, lakini tumekaa chini na
kuzungumza na uongozi na kufikia sehemu nzuri ndiyo maana mpaka sasa
niko hapa”
“Nilistushwa na uamuzi ambao ulichukuliwa na klabu yangu kwasababu
sikutarajia kitu kama hicho kingetokea, kiukweli nilikuwa surprised na
niliumizwa na uamuzi huo lakini nashukuru mambo haya yamefikia hatua
nzuri”.
Msemaji wa Yanga Jerry Muro amesema uongozi wa klabu yake unajipanga
kutoa taarifa rasmi kuhusu suala la Niyonzima ambayo itahitimisha
mjadala kuhusu kiungo huyo.
“Sisi kama uongozi wa Yanga, tunamshukuru Niyonzima kwa kuwa
muungwana juu ya hili suala na kuamua kuja kwa uongozi wa Yanga na
kuomba radhi kwa yote yaliyotokea”, amesema Muro.
“Niyonzima kwetu ni kama mtoto kwa hiyo uongozi umekaa na kuzungumza
naye na utatoa taarifa rasmi hivi karibuni na kuhitimisha mjadala wa
mchezaji huyo”.
Haruna Niyonzima alifungashiwa virago na uongozi wa Yanga kutokana na
sababu za utovu wa nidhamu ambao umekuwa ukijirudia kila mara hasa
kuchelewa kurudi pindi anapokweda nyumbani kwao kuitumikia timu yake ya
taifa au anapokuwa kwenye mapumziko ya likizo.