Madiwani watatu wa Chadema Manispaa ya Iringa wameamua kuachia nafasi zao kwa madai ya mwenendo mbaya wa chama.
Madiwani
hao walichukua uamuzi huo baada ya kumwandikia barua ya kujiuzulu
mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa. Madiwani ambao
wamechukua uamuzi huo ni Baraka Kimata wa Kata ya Kitwiru na wawili wa
viti maalumu; Husna Ngasi na Leah Mlelewa.
Wakizungumzia uamuzi huo, viongozi hao walisema kuwa wameamua kufanya hivyo baada ya kuchoshwa na mwenendo wa chama hicho.
Kimata alisema anaendelea na kazi zake nje ya siasa na kwamba, hatabaki na nafasi yoyote ndani ya chama hicho.
Alisema kuwa ushirikiano mdogo kati yake na mbunge wa jimbo hilo umemsukuma kuachia nafasi yake hiyo.
Kwa
upande wake, diwani mwingine ambaye alikuwa katibu wa Baraza la Vijana
la Chadema (Bavicha), Mlelewa alisema hatabaki na nafasi yoyote ndani ya
chama hicho kama ilivyo kwa Kimata.
Madiwani
wengine wa Chadema ambao walijiuzulu kutoka Jimbo la Arumeru Mashariki
ni Anderson Sikawa, Emmanuel Mollel, Greyson Isangya na Josephine Mshiu
pamoja na diwani wa Murieti, Credo Kifukwe.