ODINGA AKIWAHUTUBIA WAFUASI WAKE
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ameapa kutorudi nyuma
baada ya kutangaza kuwa hatambui ushindi wa rais Uhuru Kenyatta.
Odinga amesisitiza kuwa kura za urais
zilizopigwa mapema wiki hii, ziliibwa na hivyo kumpa ushindi rais
Kenyatta. Odinga anasema yeye ndio aliyeshinda Uchaguzi huo.
Kiongozi huyu mwenye umri wa miaka 72,
amewahotubia wafuasi wake siku ya Jumapili katika mtaa wa Kibera jijini
Nairobi na kuwataka kutoenda kazini kuanzia siku ya Jumatatu.
“Nawaomba wafuasi wangu, kesho msiende kazini,” amesema Odinga.
"Serikali ya Jubilee imemwaga damu, imewauwa watu wetu bila hatia," amesisitiza.
Aidha, amewataka wafuasi wa NASA
kutokabiliana na Polisi, wakati huu ripoti zikieleza kuwa watu 16
wameuawa katika mtaa wa Kibera, Mathare jijini Nairobi, Kisumu, Siaya na
Homabay baada ya kupigwa risasi na polisi wakiandamana kupinga ushindi
wa Kenyatta.
Odinga amekuwa akihimizwa kwenda Mahakamani, kupinga matokeo ya Kenyatta kama katiba inavyoeleza lakini amesema hatafanya hivyo.
Wakati akiwahotubia wafuasi wake,
waliokuwa wakiimbia na kusema bila Raila, hakuna amani na Uhuru lazima
aondoke, ameishutumu serikali kwa kuwauwa wafuasi wake wasiokuwa na
hatia kwa kutumia maafisa wa polisi na wanajeshi.
Odinga ameahidi kutoa mwelekeo wake rasmi siku ya Jumanne.