Bw Joseph Kabila ametangazwa mshindi wa urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kulingana na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo Joseph Kabila ameshinda kwa asilimia 48, mpinzani wake mkuu Etienee Thisekedi akiwa na asilimia 32.33 na Vital Khemere naye akipata asilimia 7.74.
Matokeo hayo yalitarajiwa kutoka siku ya Jumanne lakini maafisa walisema matatizo ya kusambaza vifaa katika nchi hiyo kubwa ndio yalisababisha ucheleweshaji huo.
Wapinzani wamelalamika kuhusu kuwepo udanganyifu na usalama umeimarishwa kwenye mji mkuu, Kinshasa, huku kukiwa na wasiwasi wa kutokea ghasia.
Polisi wa kuzuia ghasia wanafanya doria kwenye mitaa ya mji mkuu huo, unaoonekana kuwa ngome ya upinzani.
Maduka mengi yalifungwa kwenye soko la Kinshasa kwa takriban wiki nzima.
Mkuu wa tume wa uchaguzi Daniel Ngoy Mulunda, " Tume huru ya uchaguzi wa taifa inathibitisha kuwa Kabila Kabange Joseph amepata kura nyingi zaidi".
Katika mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo, watu walianza kushangilia matokeo tu yalipotangazwa katika televisheni na redio ya taifa, ameripoti mwandishi wa BBC Joshua Mmali.
Matokeo hayo bado yanahitaji kuidhinishwa na mahakama kuu.
Bw Kabila amekuwa rais tangu mwaka 2001, kufuatia kifo cha baba yake Laurent.
Mwaka 2006 alishinda uchaguzi wa kwanza tangu kumalizika kwa mgogoro wa miaka mitano na sasa anatarajiwa kuapishwa Desemba 20 kwa muhula wake wa pili.