Timu ya soka ya Mbeya City.
HATMA ya
safari ya timu ya Mbeya City kutoka jijini Mbeya kuelekea Sudan kwa ajili
ya kushiriki mashindano mapya ya Kombe la Nile Basin ambayo yanatarajiwa kuanza
leo mjini Khartoum haijajulikana imeelezwa.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, amesema kuwa hadi leo mchana
walikuwa hawajapokea tiketi hizo za kuelekea Sudan ili kupeperusha vyema
bendera ya Tanzania Bara katika mashindano hayo.
Kimbe alisema kuwa timu yao inaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume,
Ilala jijini na mara safari hiyo itakapokamilika wataondoka kuelekea Sudan.
Hata
hivyo inaelezwa kuwa Chama cha Soka cha Sudan (SFA) ndiyo wanaotakiwa
kushughulikia tiketi za timu na viongozi wanaoelekea nchini humo kwa
kushirikiana na serikali yao iliyodhamini michuano hiyo.
Mechi za ufunguzi za mashindano hayo leo zitakuwa ni kati ya Victoria
University dhidi ya Malakia na baadaye usiku wenyeji El Mereikh itawakaribisha
Polisi kutoka Uganda timu hizo zote ziko kundi A.
Timu nyingine zinazoshiriki mashindano hayo zilizoko kundi C ni pamoja na Al
Ahly Shandy, Al Masry ya Misri, Defence na Dhikil huku kundi D likiwa na Hey Al
Arab, Arab Contractors, Flam beaude L'EsT ya Burundi na Etincelles ya jijini
Kigali, Rwanda.
Mbeya City ambayo iko kundi B inatakiwa kuanza kampeni za kuwania ubingwa huo
kesho Alhamisi kwa kuwavaa El Mereikh Al Fashery na baadaye kucheza na AFC
Leopald ya Kenya Mei 25 na kumaliza mechi zake za hatua ya makundi kwa kukutana
na Elman ya Somali Mei 27.
Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry