Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
imesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa hawana
sifa za kugombea tena uongozi wa chama hicho kwa kuwa wanabanwa na katiba yao.
Akizungumza jana ofisini kwake baada ya
kuzungumza na Mbowe, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza alisema walipata malalamiko
na kuyafanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kupitia kumbukumbu walizonazo na kubaini
kuwa kipengele cha ukomo wa uongozi kiliondolewa kinyemela katika katiba ya
chama hicho.
Alisema kwa kawaida vyama vyote
vinapofanya mikutano huwapelekea muhtasari, hivyo Chadema nacho kiliwapelekea kumbukumbu
ya Mkutano Mkuu wa mwaka 2006, lakini hakuna sehemu yoyote iliyoondoa ukomo wa
uongozi.
“Hivyo, hawa tayari wana vipindi
viwili, wakichaguliwa katika uchaguzi unaokuja hatutawatambua. Wakitaka
wabadili katiba kwa njia halali ambayo ni ya mkutano mkuu na si vinginevyo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mbowe
alisema hakuwa tayari kulizungumzia, akieleza kwamba amefika kwenye ofisi hiyo
ya Msajili kwa masuala mengine.
“ Siwezi kulizungumzia suala hilo kwa
sasa, likifikishwa kwenye Kamati Kuu ndipo nitalielezea,” alisema Mbowe.
Baadaye Ofisa wa Habari wa Chadema,
Tumaini Makene alisema kwamba Msajili alimwita Mbowe ili kumshawishi asaidie wajumbe
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) warejee katika Bunge la Katiba.
“Mwenyekiti alibainisha kuwa msimamo wa
Ukawa upo wazi kwamba hawatarudi katika Bunge hilo hadi pale maoni ya wananchi
yatakapoanza kujadiliwa na msimamo huo hautabadilika,” alisema Makene
akimkariri Mbowe.
Makene alisema baada ya kutoa msimamo
huo, hakuna maongezi mengine yaliyoendelea baina ya Mbowe na Msajili.
Alipoulizwa iwapo Msajili alionyesha
nia pia ya kuushawishi upande wa pili wanaotaka serikali mbili, Makene alisema
hawezi kufahamu, japo kwa nafasi yake, Mutungi ana uwezo wa kufanya hivyo.
Alipoulizwa iwapo Msajili pia
alizungumzia suala la ukomo wa uongozi linalodaiwa kubadilishwa kinyemela,
alisema: “Kuhusu hilo Chadema tunafuatilia kwa kina taarifa zinazozagaa zikionyesha
correspondence (barua) zinazotoka kwa Msajili wa Vyama juu ya Chadema na
tutakapokamilisha tutatoa taarifa.”