UKAWA WASEMA HAWAYATAMBUI MATOKEO YA URAIS YANAYOTANGAZWA NA NEC.
Chadema
kwa kushirikiana na vyama vinavyounda Ukawa, leo wanakutana kujadili
mwenendo waliouita usio halali wa kutangaza matokeo, wakiituhumu Tume ya
Uchaguzi (NEC), CCM na Jeshi la Polisi kushirikiana kuhujumu matokeo.
Viongozi
hao wa Ukawa, Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, James
Mbatia (mwenyekiti, NCCR Mageuzi) na Profesa Abdallah Safari, ambaye ni
mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema walizungumza na waandishi wa habari jana
Makumbusho jijini Dar es Salaam na kusema hawayatambui matokeo
hayo kwa kuwa yamechakachuliwa.
Mbowe
aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kuna vijana kutoka Kenya,
ambao wamewekwa hoteli mmoja Dar es Salaam ambao wanafanya kazi ya
kuchakachua matokeo yanayotoka majimboni na baadaye kuyapeleka NEC.
“Ndio maana matokeo yaliyopo kwenye fomu za mawakala wetu yanatofautiana na matokeo yanayotangazwa na NEC,” alisema mwenyekiti huyo wa Chadema.
Aliyataja baadhi ya majimbo hayo kuwa ni Nyamagana, Rungwe, Kahama Mjini, Shinyanga Mjini, Kyela na Muleba Kusini.
“Kazi hii ya uchakachuaji matokeo inafanywa na CCM, inaratibiwa na NEC na wasimamizi wakubwa ni polisi,” alisema Mbowe.
Akichangia suala hilo, Profesa Safari alitoa mfano wa Jimbo la Tandahimba ambako alisema NEC ilitangaza kuwa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli alipata kura 49,098 na Lowassa kura 46,288 ambazo ni tofauti ya kura 280.
“Lakini matokeo halisi kutoka kwa mawakala wetu yanaonyesha Lowasa alipata kura 44,537 na Dk Magufuli 44,253 ambazo ni tofauti ya kura 284,” alisema Profesa Safari.
Pia alisema NEC ilitangaza kuwa Lowassa alipata kura 6,000 Jimbo la Tunduma, wakati matokeo yao yanaonyesha alipata kura 32,442.
Mbowe
pia alizungumzia vijana 191 waliokamatwa na polisi, ambao nane kati yao
walifikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka ya kufanya makosa ya
kimtandao.
“Kitendo kilichofanywa cha kuwanyima dhamana ni cha kinyama hakistahili,” alisema Mbowe.
“Kwanza kuna wageni wawili ambao hawahusiki kabisa na shughuli za ujumlishaji matokeo ya Chadema.”
Alisema
kitendo cha polisi kuwakamata vijana hao waliokuwa wakijumlisha
matokeo, kimevuruga mfumo wa ukusanyaji matokeo wa Chadema.
“Lakini
sasa tunatumia fomu za mawakala wetu ambazo zinaonyesha (mgombea urais
wa Chadema, Edward) Lowassa anaongoza kwa tofauti kubwa ya kura,” alisema Mbowe.
Alisema
vijana hao wamekamatwa kwa kosa ambalo linafanywa na mjumbe wa Kamati
ya Kampeni ya CCM, January Makamba ambaye Mbowe alisema amekuwa
anatangaza matokeo ya uchaguzi na idadi ya majimbo bila ya kuchukuliwa
hatua zozote.
“Huu si uchaguzi, ni uchafuzi,” alisema Mbowe.
Hata
hivyo, Makamba alisema jana kuwa hakuna tatizo la yeye kusema kuwa
watashinda kwa asilimia fulani kwa sababu kila chama kimekuwa kikisema
hivyo.
“Hali
hii inatufanya tuamini sababu za NEC kuchelewesha Daftari la Wapigakura
na kutoruhusu wapinzani kukagua mfumo wa kujumlisha matokeo.”
Mbowe alisema wanalazimika kujadili sasa suala hilo kwa kuwa katiba hairuhusu matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani.
Alisema Kamati Kuu ya Chadema inakutana leo jijini Dar es Salaam kujadili suala hilo na kutoa tamko na pia kikao cha viongozi wa Ukawa kitakutana leo kutoa mwelekeo wa uchaguzi.
Akizungumza
kwenye mkutano huo na waandishi, Mbatia alisema: “Hili ni janga la
Taifa linalotengenezwa na binadamu huku wakijua athari zake.
“Nchi
ni mali ya watu wote na ukawa hawataki machafuko. NEC ikiendelea
inaweza kukamilisha ile kauli kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa si
huru.”
“Unaweza kuchakua matokeo lakini huwezi kuchakachua hisia za Watanzania,” alisema Mbatia.
Alisema
kinachotokea ni kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukataa mapendekezo ya
vyama vya upinzani waliomtaka abadili mambo manne kwenye katiba kabla ya
uchaguzi.
Aliyataja
mamnbo hayo kuwa ni matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, kuruhusiwa
kwa mgombea binafsi, mgombea urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50 na
tume ya uchaguzi kuwa huru.