Taarifa kutoka Sudan Kusini iliyotolewa na Umoja wa Mataifa nchini humo inaeleza kuwa watoto wanajeshi zaidi ya 300 wameachiwa huru na vikundi vya mapigano nchini humo.
Watoto hao 311, kati yao 87 wakiwa ni wasichana wataanza kurudishwa kwenye familia zao siku za hivi karibuni. Inaelezwa kuwa hadi sasa watoto 2,000 wameshaachiwa na vikundi hivyo na 10% kati yao wako chini ya umri wa miaka 13.
Inategemewa kuwa watoto 700 wengine wataachiwa huru wiki ijayo. Watoto takribani 19,000 wanahisiwa kutekwa na vikundi hivyo kutoka maeneo mbalimbali nchini humo. Watekaji hao huwafundisha watoto hao kutumia silaha za moto.
Mkuu wa UN nchini humo David Shearer kwenye taarifa hiyo amenukuliwa akisema “watoto hawatakiwi kubebeshwa silaha na kuuana, wanatakiwa wacheze, kusoma na kufurahi na rafiki zao huku wakilindwa na kufurahiwa na watu wazima wanaowazunguka.”