Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na
Vijana, Anthony Mavunde alibaini kuwepo kwa wafanyakazi wa kigeni katika
makampuni hayo walioajiriwa kufanya kazi za kufunga meza na viti, kazi
ambazo hata watanzania wangeweza kuzifanya.
“Lakini pia kuna wageni ambao wako katika hii kampuni yenu, wanafanya
kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania, kwa mfano huyu anayefunga
viti, hii kazi inafanywa na vijana wetu…kibali chake kinaisha kesho,
naagiza asipewe kingine na aondoke,” Mavunde anakaririwa.
Katika ziara yake iliyolenga kufanya ukaguzi wa vibali vya ajira kwa
wageni, Mavunde alibaini pia uwepo wa raia wa Vietnam wanaofanya kazi
katika kampuni ya simu ya Halotel bila kuwa na vibali vya kuishi nchini
wala vibali vya kufanya kazi.
Pia, alibaini uwepo wa wafanyakazi wa
kampuni hiyo ambao hawajapewa mkataba wa ajira huku waliopewa mikataba
ya ajira hawakupewa nakala ya mikataba yao kinyume cha sheria.
Baada ya kubaini uwepo wa mapungufu hayo, Mavunde aliagiza uongozi wa
Halotel kuhakikisha wanawapa mikataba wafanyakazi wao wote na kuzipeleka
nakala za mikataba hiyo ofisini kwake.