JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898 OFISI YA RAIS IKULU
1, BARABARA YA BARACK OBAMA
11400 DAR ES SALAAM
TANZANIA
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti :
www.ikulu.go.tz Faksi: 255-22-2113425
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli,
amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)
Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu Mstaafu
Plasdus Gervas Nkalanga (OSB) kilichotokea Ijumaa tarehe 18 Desemba,
2015 katika hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho, Wilaya ya Songea
Mkoani Ruvuma.Mhashamu Askofu Nkalanga
aliyekua Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba alistaafu uaskofu mwaka 1974
na kujiunga na watawa wabenediktini wamonaki ambapo aliamua kwenda
kuishi katika Abasia ya Hanga iliyopo katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani
Ruvuma. Katika salamu zake Rais Magufuli
amesema Askofu Nkalanga aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96
atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kuhimiza imani na
uchapakazi kazi katika kipindi chote cha miaka 54 ya uaskofu wake na
utawa wake akiwa katika Abasia ya Hanga.Amesema Marehemu Askofu Nkalanga ambaye baada ya kustaafu aliamua kuingia katika utawa akianzia katika ngazi ya chini kabisa ya Unovisi hadi
alipofunga nadhili za milele za utawa mwaka 2009, ameacha mfano mzuri
unaohimiza jamii kuishi kwa upendo, unyenyekevu na kutokata tamaa. "Kupitia
kwako Baba Askofu Ngalalekumtwa napenda kuwapa pole nyingi Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Abate wa Abasia ya Hanga, watawa na
waumini wote wa kanisa Katoliki kwa kupoteza mtu muhimu aliyetoa mchango
mkubwa katika maendeleo ya kanisa na jamii kwa ujumla" amesema Rais
Magufuli.Rais John Pombe Magufuli amemuomba
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu Mhashamu Askofu Mstaafu
Plasdus Gervas Nkalanga mahali pema peponi, Amina.Gerson MsigwaKaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU