Mkurugenzi mkuu wa shirika la ndege
la Air France amefutilia mbali tahadhari ya bomu iliyosababisha ndege ya
kutua Kenya kuwa ni ya uongo
Frederic Gagey amewaambia waandishi
wa habari mjini Paris Ufaransa kuwa kifaa kilichodhaniwa kuwa kilipuzi
kilikuwa ni mbao na kisanduku cha karatasi tu wala haikuwa na hatari
yeyote kwa usalama wa ndege hiyo.
-
Ndege hiyo ya abiria ya Air France Boeing 777 AF463, inayohudumu
kati ya Mauritius na Paris ililazimika kutua kwa ghafla katika uwanja wa
ndege wa kimataifa mjini Mombasa - Kenya baada ya kifaa kinachodhaniwa
kuwa bomu kupatikana ndani ya choo cha ndege hiyo.
-
Inasemekana kuwa abiria mmoja alikipata kifaa hicho chooni na akamfahamisha mhudumu mmoja wa ndege hiyo.
Mhudumu huyo alimfahamisha rubani kuhusiana na kifaa hicho na shughuli za kutua kwa dharura zikaanza.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria 459 na wahudumu 14.
Ndege
hiyo ilitua saa sita usiku wa kuamkia leo Jumapili, huku wataalamu wa
kutegua mabomu kutoka jeshi la wanamaji la Kenya wakiingia ndani ya
ndege hiyo kukagua kifurushi kilicholeta taharuki.
Sasa kitengo cha ujasusi cha Ufaransa kimeanzisha uchunguzi wa kina kubaini kilichosababisha tishio hilo.