Saudi
Arabia imesema nchi 34 zimekubaliana kuunda muungano wa kijeshi wa
kiislamu kupambana dhidi ya ugaidi ambapo operesheni za pamoja zitakuwa
zikiratibiwa kutoka mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
Tangazo
hilo limechapishwa na shirika la habari la Saudi Arabia na kuongeza
muungano huo utaongozwa na nchi hiyo na umeanzishwa kwa sababu ugaidi
unapaswa kukabiliwa kwa kutumia kila njia na ushirikiano huo utakuwa
njia mwafaka utakao uangamiza.
Taarifa
hiyo inasema Uislamu unapinga ufisadi na maangamizi na ugaidi unakiuka
hadhi na haki za binadamu hasa haki ya kuishi na kuwa salama. Miongoni
mwa nchi zitakazoshiriki katika muungano huo ni Pakistan, Uturuki,
Misri, Libya na Yemen. Mali, Chad, Somalia na Nigeria pia ni wanachama
wa muungano huo mpya wa kupambana dhidi ya ugaidi.
Hasimu wa
muda mrefu wa Saudi Arabia, Iran haijajumuishwa katika muungano huo.
Saudi Arabia na Iran zimekuwa zinayaunga mkono makundi tofauti katika
mizozo ya Yemen na Syria. Oman pia haijashirikishwa katika muungano huo
wa kijeshi.