Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) Dkt Edward Hoseah, na pia amewasimamisha kazi
maafisa wa nne wa taasisi hiyo.
Rais Magufuli amesema
hajaridhishwa "na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake
katika kukabiliana na rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya
serikali katika bandari ya Dar es salaam.”
Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Ombeni Sefue amesema Dkt Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Bw Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Takukuru.
Kwa mujibu wa Bw Sefue, Dkt Magufuli amechukua
hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa "utendaji kazi wa Takururu chini
ya Dkt Edward Hoseah hauwezi kuendana na kazi anayoitaka”.
Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi
waandamizi wanne wa Takururu ambao walisafiri nje ya nchi licha ya Rais
Magufuli kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.
Watumishi
hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas
ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka
kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Bw Sefue amesema atakayekiuka agizo la rais "atachukuliwa hatua kali”.
Hii
si mara ya kwanza kwa Dkt Magufuli kuwachukulia hatua maafisa wa
Serikali tangu achukue madaraka mwezi uliopita. Siku chache baada ya
kuingia ofisini, alibadilisha usimamizi wa hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kufanya ziara ya kushtukiza huko na kutoridhishwa na utoaji huduma.
na juzi alivunja
bodi inayosimamia bandari Tanzania.