Zaidi ya
wachungaji hamsini wa kanisa la Anglikana Tanzania dayosisi ya Victoria
Nyanza (DVN) wametangaza kumfukuza kazi ya uaskofu, askofu Boniface
Kwangu wa dayosisi hiyo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na
ubadhirifu wa fedha pamoja na mali za kanisa hilo.
Tamko
hilo la Wachungaji 53 wa dayosisi hiyo limesomwa mbele ya waumini wa
Kanisa Kuu la Mtakatifu Nicholas wakati wa ibada ya Jumapili na
Mchungaji Andrew Kashilimu, ambaye pia ni mwenyekiti wa nyumba ya
wahudumu.
Kufukuzwa
kazi ya uaskofu kwa askofu Kwangu aliyehudumu katika dayosisi hiyo kwa
miaka minane, kuanzia mwaka 2008 hadi kufikia leo, kunafanya jumla ya
maaskofu waliowahi kufukuzwa na kanisa hilo kuwa wawili, akiwemo
mtangulizi wake marehemu John Changaye ambaye alifukuzwa uaskofu mwaka
2007 kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha na mali za kanisa.
Askofu Kwangu amevuliwa wadhifa huo akiwa nchini Marekani ambako amekaa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Kanisa la
Anglikana Tanzania dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) lina jumla ya
wachungaji sitini na zaidi ya waumini laki sita katika makanisa yake.