Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Naibu
Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee,
Dkt. Hamisi Kigwangalla ameanzisha kikosi kazi cha watu 24 ambacho
kitakuwa na kazi ya kutengeneza mpango mkakati wa kuwezesha kuboresha
Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Katika taarifa ambayo imetolewa na
Dkt. Kigwangala imeeleza kuwa kazi ya kuanzisha kikosi kazi hicho ni
agizo kutoka kwa Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ambaye alimtaka aanzishe kikosi hicho ili
washirikiane kuanzisha mpango mkakati wa kuwezesha kuboresha Mfuko wa
Afya ya Jamii.
“Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu alinipa kazi ya kuunda kikosi kazi
maalum na kushirikiana nacho kutengeneza mpango mkakati wa kuboresha
Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF),” alisema Dkt. Kigwangalla.
Dkt.
Kigwangalla amewataja wajumbe wa kikosi kazi hicho kuwa ni Prof. Angwara
Kiwara, Prof. Phares Mujinja, Dkt. Francis Frederick, Dkt. Heri Marwa,
Dkt. Deogratius Pisa, Dkt. Amos Kahwa, Irenei Kiria, Semkae Kilonzo,
Gemini Mtei, Dkt. Jehovaness Aikaeli na Obey Assey.
Wengine ni
Mathias Kabunduguru, Dkt. Dereck Chitama, Prof. Flora Kessy, Florence
Mwanri, Athuman Rehani, Maximillian Mapunda, Bedason Shallanda, Daniel
Ngowi, Beng' Issa, Edwin Mikongoti, Hussein Sengu, Dkt. Beatus Leon na
Dkt. Pastory Sekule.
Aidha Dkt. Kigwangalla amewashukuru wajumbe
hao kwa kukubali kufanya kazi na Wizara ya Afya kupitia mpango mkakati
wa kuwezesha kuboresha Mfuko wa Afya ya Jamii bila malipo yoyote.
Hata
hivyo mara baada ya kuwachagua wajumbe wa kikosi kazi hicho tayari
kimependekeza mapendekezo yao jinsi ya kuboresha Mfuko wa Afya ya Jamii
ambayo ni kuipa nguvu kadi ya CHF ili itumike kwenye mfumo wa Afya mpaka
ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na vituo vya Jirani na kupandisha
kiwango cha kuchangia CHF mpaka 30,000.
Mapendekezo mengine ni
kuweka bei za kukatisha tamaa watumiaji wa huduma za Afya bila kadi ya
Bima ya Afya ama ya CHF na kuwahamasisha waamue kujiunga kuliko kulipa
gharama za kila huduma watakayotumia, kuhamisha Mfuko wa fedha za CHF
kutoka Halmashauri na kuupeleka NHIF ngazi ya mkoa lengo likiwa
kumtenganisha mtoa huduma na mteja na kuweka 10,000 kuwa kiwango cha
chini kwa bei za huduma za afya sehemu yoyote nchini kwa mtu asiye na
kadi.
Aidha mapendekezo yao yatatumika kama serikali itayaridhia
na wao wametoa mapendekezo hayo kutokana na kutambua kuwa Watanzania
wapo tayari kulipia huduma za afya kwa bima ilimradi wawe wanapatiwa
huduma bora ambazo zitawaridhisha.