Katika
kuhakikisha inarejesha makali yake, uongozi wa Simba umemsainisha kocha
wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Hemed Suleiman Morocco
ambaye anakuja ‘ku-boost’ benchi la ufundi linaloongozwa na Mganda,
Jackson Mayanja.
Morocco
amefundisha klabu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Coastal Union, JKT
Oljoro na Zanzibar Heroes iliyo chini ya nahodha Nadir Haroub
‘Cannavaro’ wa Yanga. Morocco pia ni Kocha Msaidizi wa Taifa Stars.
Taarifa
za uhakika kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya Simba, zimesema
Morocco anakuja kuwa mshauri mkuu wa benchi la ufundi ambako ameanguka
saini ya miezi sita.
Chanzo makini kimeeleza anatarajiwa kuanza kazi leo Jumatatu.
Alipofuatwa
Morocco na kuuliza taarifa za kuanguka saini Msimbazi akakiri kuwa ni
kweli na muda wowote anatarajia kuanza kibarua baada ya kufikia
makubaliano mazuri na uongozi wa Simba.
Lakini
akashindwa kubainisha kama atabwaga manyanga kuinoa Stars akidai
wanaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kujua hatima yake baada ya kupata ulaji mpya.
“Wakati wowote natarajia kuanza kazi, baada ya kufikia makubaliano mazuri na viongozi wa Simba,” alisema Morocco.
Alipoulizwa
Katibu Mkuu wa Simba, Enock Kiguha, alikiri kuwa wamemalizana na kocha
huyo lakini akadai suala la muda wa mkataba linabaki kuwa siri ya klabu.
“Tumeingia mkataba na Morocco. Ataanza majukumu yake muda si mrefu,” alisema katibu huyo kwa ufupi.