Chama cha
Mapinduzi CCM Mkoani Mwanza, kimewataka viongozi mbalimbali Mkoani
Mwanza, kuwatumikia vema wananchi waliochagua na kuacha kufanya kazi kwa
mazoea.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Katibu Mwenezi wa Chama hicho Simon Mangellepa
mbele ya wanahabari, wakati akitoa shukrani kwa makundi mbalimbali ya
wananchi ambayo ni pamoja na machinga, wakulima, wavuvi pamoja na
wafanyabiashara kwa namna walivyojitoka kwa hali na mali kukisaidia
chama hicho kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka
jana.
Mangellepa
amesema kuwa uchaguzi umemalizika hivyo ni vema viongozi wote ambao ni
pamoja na Mabalozi, Wenyeviti wa Serikali za Mtaa na Vijiji, Madiwani
pamoja na Wabunge wakaacha kuwatumikia wananchi kwa mazoea na badala
yake wawakilishe vizuri katika ngazi za maamuzi katika kutatua matatizo
yao.
“Hii
kauli ya Hapa Kazi Tu haishii kwa Magufuli peke yake (Rais John Pombe
Magufuli), mimi nasema inaanzia hata kwa mabalozi, wenyeviti wa
vitongoji, mitaa, madiwani na wabunge. Chama cha Mapinduzi Mkoa
kinawataka Madiwani na Wabunge warudi kwa wananchi ili wanapokwenda
kuwawakilisha wananchi wawakilishe mawazo sahihi ya wananchi wao”.
Alisema Mangellepa.
Kauli
ya Chama hicho imeungwa mkono na baadhi ya wananchi Jijini Mwanza ambao
wamewakumbusha viongozi wao kuhakikisha kwamba wanatatua changamoto
zinazowakabili ambazo ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana, ubovu wa
miundombinu, kushughulikia kero ya upatikanaji wa maji safi na salama
pamoja na huduma za afya katika ngazi za Kata ili kutimiza ahadi
walizozitoa wakati wa kampeni zao.
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mwanza Simon Mangellepa akiongea na Wanahabari katika ofisi za Chama hicho Mkoa wa Mwanza.