Mwongozo huo mpya pia unapiga marufuku wahubiri kutafuta wafuasi kupitia vipindi redioni na runingani
Mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya imechapisha mwongozo mpya wa vipindi vya radio na televisheni.
Mwongozo
huo unanuia kudhibiti nyakati za kupeperusha matangazo na vipindi
vinavyolenga watu wazima na pia kuepusha matumizi ya lugha chafu na
gumzo za ngono.
Mwongozo
huo utakapotekelezwa pia utapiga marufuku kupeperushwa kwa vipindi vya
kidini vyenye ujumbe wa kuomba pesa kwa waumini ili wapate baraka.
Mwaka
uliopita, mhubiri mmoja aligonga vichwa vya habari baada ya makala ya
ufichuzi kuonyesha akifanya miujiza bandia na kuwaomba watu wamtumie
takriban $3 (£2) kupitia simu akisema ni baraka ndipo wapate baraka.
"Wahubiri
hawafai kutumia dini kufaidi kutoka kwa watazamaji au wasikilizaji kwa
kuwaomba wawasaidie kifedha au kushambulia imani ya mtu kwa kumshawishi
mtu kubadili imani yake," mwongozo huo unasema.
Vipindi
vya redio vinavyozungumzia ngono au masuala ya watu wazima, au kutumia
lugha chafu pamoja na video zenye picha za uchi vyote havifai
kupeperushwa kati ya saa kumi na moja asubuhi na saa nne usiku.
Hii ni mara ya kwanza hatua kama hiyo kuchukuliwa.
Kaimu
mkurugenzi wa masuala ya wateja katika Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya
Bw Christopher Wambua anasema mwongozo huo umeandaliwa baada ya
majadiliano kati ya wadau mbalimbali mwaka jana.
"Mamlaka
ilianza kutoa leseni za TV kwa mashirika mbalimbali baada ya kumalizika
kwa kesi mahakamani ambayo ilikuwa imewasilishwa kupinga mamlaka ya
mamlaka hiyo katika kudhibiti utangazaji. Mwongozo huu ni sehemu ya
masharti ambayo watangazaji wanafaa kutii," Bw Wambua ameambia BBC.
"Mamlaka imewapa watangazaji miezi sita ya kutekeleza mwongozo huu. Muda huu utamalizika katikati mwa mwaka huu."BBC