Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemwandikia
barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akisema Wasaudi Arabia wanapaswa
kuchagua moja baina ya kuendelea kuyaunga mkono makundi yenye misimamo
ya kufurutu mipaka au kufanya jitihada za kuimarisha amani katika
Mashariki ya Kati.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema katika barua hiyo iliyotumwa
kwa Ban Ki-moon jana Ijumaa kwamba Saudi Arabia inapaswa kuchagua moja
kati ya mambo mawili, ama kuendelea kuyaunga mkono makundi yenye
misimamo mikali na kuchochea chuki na uhasama wa kimadhehebu au
kuimarisha ujirani mwema na amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Dakta Zarif ameongeza kuwa, Iran haitaki kuzidisha mivutano katika
nchi jirani na inatarajia kuwa Saudi Arabia pia itafuata njia ya
mantiki.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema tangu siku za mwanzoni mwa
kuchaguliwa Rais Hassan Rouhani na kuanza kazi serikali ya awamu ya 11
hapa nchini, Tehran iliitumia ujumbe serikali ya Riyadh kwa lengo la
kuimarisha ushirikiano na mazungumzo ya kuboresha amani na usalama wa
Mashariki ya Kati na vilevile kukabiliana na misimamo mikali na makundi
yanayofurutu mikapa.
Waziri Zarif amesema badala yake wakuu wa Saudia
walifanya kila wawezalo kukwamisha jitihada za kufikiwa mapatano ya
nyuklia kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1.