Rais wa
Sudan Kusin Salva Kiir ameteua wabunge 50 kutoka vuguvugu la waasi na
kukubali kugawanya nyadhifa za uwaziri na wapinzani wake kulingana na
mkataba wa amani unaonuia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe .
Kwenye tangazo kupitia radio ya serikali ya nchi hiyo,Kiiir ametangaza uteuzi wa wabunge 50 waliopendekezwa na upande wa waasi.
Rais wa
zamani wa Botswana Festus Mogae ambaye anaongoza tume ya pamoja ya
kufuatilia na kutathmini iliyoundwa na jumuiya ya IGAD kuhakikisha
mkataba huo unatekelezwa,amesema serikali itapewa nyadhifa 16 za uwaziri
zikiwemo za ulinzi,usalama wa kitaifa,fedha na sheria huku waasi
wakipewa nyadhifa 10 zikiwemo za mafuta na maswala ya kibinadamu.
Wafungwa wa zamani kupokea nyadhifa
Kundi la
wanasiasa wenye ushawishi mkubwa lijulikanalo kama wafungwa wa zamani
ambao walifungwa wakati mapigano yalipoanza lakini wakaachiliwa
baadaye,watapokea wadhifa wa maswala ya nchi za kigeni na ule wa
uchukuzi huku nyadhifa za maswala ya baraza la mawaziri na kilimo
zikiendea vyama vingine vya kisiasa.
Pande
zote mbili za serikali na waasi kwenye mzozo huo wa miaka miwili nchini
Sudan Kusini zimelaumiwa kwa kuchochea mauaji ya kikabila,kusajili na
kuwauwa watoto na kutenda visa vya unajisi,mateso na kuhamisha watu kwa
nguvu ili kuwaondoa maeneo ya wapinzani wao.
Mzozo huo
umesababisha mzozo wa kibinadamu huku watu milioni 2.3 wakilazimika
kuhama makwao na wengine milioni 4.6 wakihitaji msaada wa chakula.Maelfu
ya watu wameuawa na uchumi kuporomoka..
Pande zote zimelaumiana kuvunja mikataba
Kiir na
kiongozi wa waasi Riek Machar wameshutumiana kwa kuvunja mikataba ya
amani lakini wanasema wangali wazingatia makubaliano ya tarehe 26 mwezi
Agosti,licha ya kushindwa kuafikia tarehe za mwisho zilizowekwa.
Chini ya
makubaliano hayo Machar anastahili kuchukua wadhifa wa makamu wa
Rais,wadhifa aliofutwa mwaka 2013.
Kiongozi huyo wa waasi hadi sasa
hajasafiri hadi Juba kuchukua nafasi hiyo.
Hakuna
muda uliyowekwa wa lini mawaziri watateuliwa na kuchukuwa nyadhifa
hizo.Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza mwei Disemba 2013 wakati Kiir
alipomlaumu Machar kwa kupanga mapinduzi,hatua iliyosababisha mauwaji
ya kilipiza kisasi ambayo yameigawanya kikabila nchi hiyo masikini.
Serikali hiyo ya muungano,itadumu kwa muda wa miaka 3 kabla ya uchaguzi kufanyika na itakuwa na wizara 30.
Wachambuzi wamepongeza hatua hiyo lakini wakaonya kuwa maswala mengi muhimu kwenye makubaliano ya amani hayajashughulikiwa.
Mwezi
uliopita Kiir alifutilia mbali mfumo wa zamani wa majimbo 10,na kuunda
maeneo mapya 28 na hivyo kuenda kinyume na mkataba wa kugawanya mamlaka.
Mapigano
yanaendelea na mzozo huo sasa unahusisha makundi kadhaa ya wapiganaji
ambayo hayazingatii mikataba iliyoandikwa ya amani,huku yakiongozwa na
ajenda za maeneo yao na mashambulizi ya kulipiza kisasi.