Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa bandari ya
Bagamoyo utasubiri hadi kukamilika kwa uongezaji wa kina cha maji katika
Bandari ya Dar es Salaam na uboreshaji wa Bandari ya Mtwara.
Profesa Mbarawa alisema
mbali ya kuongeza kina katika bandari ya Dar es Salaam, pia kipaumbele
kikuu ni kujenga gati namba 13 na 14 zinazopigiwa kelele.
Akizungumza jana katika
ofisi za Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Profesa Mbarawa alisema
mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam,
gati namba moja hadi namba saba zinaongezwa kina cha maji ili kuongeza
ufanisi.
Alisema lengo la ziara yake katika ofisi hizo ni kujifunza na kuzungumza na wafanyakazi huku akisisitiza uwajibikaji.
Akielezea kuhusu kukwama kwa
kivuko cha Mv Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi
Joseph Nyamhanga alisema ni miundombinu ya kukiendesha ikiwamo vituo kwa
ajili ya kupandisha na kushusha abiria.
Alisema tayari fedha zimepatikana na wanaanza ujenzi wa kituo cha kwanza eneo la Jangwani Beach na baadaye Ununio.