
WAZIRI MKUU WA TANZANIA KASSIM MAJALIWA
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika
ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko
kwa ngozi za wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 18, 2016) wakati akizungumza
na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika
kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone,
Botswana.
Waziri Mkuu alikuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku
moja kumwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC
Double Troika yaani kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC
Summit) na Wakuu wa Nchi wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa,
Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security
Cooperation) uliofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC),
jijini Gaborone, Botswana.
Akizingumza na Watanzania hao, Waziri
Mkuu alisema: “Tumeamua kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye
mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam (kule Pugu) ili ngozi
zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani,” alisema.
Alisema
Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini kama njia mojawapo ya kukuza
uchumi, kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira
kwa Watanzania.
Akijibu hoja zilizoainishwa kwenye risala yao,
Waziri Mkuu alisema Serikali bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba
itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi zijenge ofisi zao
Dodoma. “Serikali ilikwishaamua kwamba Dodoma ni mji wa kiserikali na
Dar es Salaam ni mji wa kibiashara. Kwa sasa kuna baadhi ya Wizara
zimeshajenga ofisi Dodoma na kuna taasisi kama vile Benki Kuu nazo pia
zimejenga ofisi zake Dodoma. Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara
nyingine zikamilishe ujenzi wa ofisi zao,” alisema.
Waziri Mkuu
Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni
(Diaspora) watafute fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa marafiki zao
ili waweze kuwekeza nyumbani (Tanzania).
“Nia ya Serikali sasa
hivi ni kufungua milango kwa wawekezaji hasa wenye nia ya kujenga
viwanda. Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza kuwekeza, kama mna
miradi huku fungueni matawi kule nyumbani. Serikali inajivunia uwepo
wenu kwa sababu inatambua kwamba huku mliko kuna kitu mnajifunza na
mnaweza kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa
ujumla,” alisema.
Mapema, akisoma risala yao kwa niaba ya
wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania waishio nchini Botswana (The
Association of Tanzanians in Botswana - ATB), Bw. Neiman Kissasi
alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na lengo la
kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu wao na
kusaidiana.
Katika risala yao, walishauri wafugaji wa Tanzania
waelimishwe na kuwezeshwa kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa
kurandaranda. Pia waliiomba Serikali iongeze kasi ya mpango wake wa
kuhamisha shughuli zote za Serikali mjini Dodoma, kwani itasaidia
kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuwa shughuli za Serikali zitakuwa
zinafanyika eneo moja.
Vilevile, waliiomba Serikali ifungue fursa
za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani,
Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya kuziacha ziwe Dar es Salaam
peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za kiuchumi na kupunguza
msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema sehemu ya risala yao.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku (Jumatatu, Januari 18, 2016.)
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, JANUARI 19, 2016.