Katika gazeti
la Tanzania Daima ukurasa wa 5, toleo namba 4070 la tarehe 25 Januari,
2016, lilichapisha habari yenye kichwa cha habari Polisi “waisoma”
namba. Sehemu ya taarifa hiyo inaeleza kuwa askari Polisi hivi sasa
wanatakiwa kujilipia gharama za umeme.
Jeshi
la Polisi nchini, linakanusha vikali taarifa hiyo kwamba siyo sahihi.
Ukweli ni kwamba askari polisi wote makambini wanalipiwa umeme na
serikali, ikiwemo wale ambao nyumba zao zimefungiwa luku kama njia ya
kuboresha huduma na matumizi sahihi ya umeme. Baada ya askari kununua
umeme hutakiwa kuwasilisha stakabadhi ya malipo ya umeme kwa ajili ya
kurudishiwa kiasi cha fedha walichonunulia umeme kila mwisho wa mwezi.
Aidha,
habari iliyochapishwa na Tanzania Daima ililenga kupotosha umma na
mwandishi wa habari hiyo hakutafuta ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka
husika.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, linamtaka
mhariri wa gazeti la Tanzania Daima na waandishi wake wa habari kuwa
makini na habari wanazoziandika hasusani taarifa zinazohusu vyombo vya
ulinzi na usalama ili kuepuka madhara ya kiusalama yanayoweza kutokea
kutokana na habari wanazozitoa zisizo na usahihi.
Imetolewa na:-
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu.