TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI
MKUU AKUTANA NA BALOZI WA FINLAND NCHINI
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Bwana Pekka Hukka.
Akizungumza na Balozi Hukka leo, alipomtembelea ofisini kwake, Magogoni
jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu amemshukuru Balozi huyo kwa namna ambavyo
nchi ya Finland imeendelea kuisaidia Tanzania na kumumwomba
waendeleze uhusiano mwema uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 50 sasa.
“Ninashukuru na kutambua
mchango wa nchi yako wa kuisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali ikwemo Utalii
na Biashara, ninashukuru sana kwa hilo” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Pia, alitumia fursa hiyo
kuwakaribisha wawekezaji kutoka Finland kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda na kuendeleza maeneo ya ukanda maalum ya
uwekezaji (EPZ) ili kuongeza thamani ya mazao pamoja na kutatua tatizo la ajira
nchini.
Waziri Mkuu, pia ameendelea
kwa kusema Serikali imedhamiria kukusanya mapato kikamilifu na kuzuia mianya ya
upotevu wake, hivyo ameiomba Serikali ya Finland isaidie katika kujenga uwezo wa
namna bora zaidi ya utekelezaji wa dhamira hiyo, kwa kuwa Finland ni kati ya nchi zenye
mifumo bora na madhubuti ya ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake, Balozi Hukka
amesema nchi yake kupitia Balozi za Tanzania na Finland zimeanza jitihada za kuandaa
utaratibu kwa ajili ya kuwekeza nchini , na kuna baadhi ya kampuni tayari ziko nchini.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, JANUARI 8, 2016.