Kipa Mcameroon wa Yanga, Youthe Rostand aliokoa penalti ya beki wa kushoto na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, lakini akashindwa kuokoa za beki Mzimbabwe, Method Mwanjali, mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi, kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, na wazawa Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim ‘Mo’.
Kwa Simba hiyo inakuwa mara ya tatu kutwaa Ngao ya Jamii tangu ilipoanzishwa mwaka 2001, baada ya kuibeba pia katika miaka ya 2011 ikiifunga Yanga pia 2-0 na 2012 ikiifunga Azam FC 3-2.
Katika mchezo wa leo, uliochezeshwa na marefa wa Dar es Salaam Heri Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Ferdinand Chacha wa Mwanza, timu zilishambuliana kwa zamu ndani ya dakika 90 za kawaida.
Lakini sifa ziende kwa safu za ulinzi za timu zote, Yanga ikiongozwa na Yondan na Simba ikiongozwa na Mwanjali pamoja na makipa wao, Manula na Rostand.
Safu ya ulinzi ya Yanga leo ilikuwa ina uhai zaidi kutokana na uhodari na ufundi wa kiungo mpya wa ulinzi, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi aliyesajiliwa kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland.
Kiungo aliyetoka Yanga kwenda Simba, Haruna Niyonzima alicheza vizuri na kutengeneza nafasi ambazo hata hivyo hazikutumiwa vizuri. Hajib pia aliyetoka Simba kuhamia Yanga, naye alicheza vizuri lakini akapoteza nafasin nzuri za kufunga.
Donald Ngoma aliisumbusa ngome ya Simba, lakini akapoteza nafasi mbili nzuri za kufunga kama ilivyokuwa kwa Okwi, naye alipoteza nafasi moja nzuri. Winga Emmanuel Martin alikaribia kuifungia Yanga kipindi cha pili baada ya kuwatoka mabeki wa Simba na kuingia na mpira kwenye boksi, kabla ya kupigiwa filimbi ya kuotea na refa Sasii. Beki mpya wa Yanga, Gardiel Michael leo alimdhibiti vizuri Kichuya.
Baada ya mchezo huo, Simba walikabidhiwa Ngao na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku Medali wakivishwa na Makamu wa Rais, Michael Wambura.
Kikosi cha Simba kilikuwa; Aishi Manula, Ally Shomari, Erasto Nyoni/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk89, Salim Mbonde, Method Mwanjale, James Kotei, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk80, Laudit Mavugo/Juma Luizio dk73, Emanuel Okwi na Haruna Niyonzima.
Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassan Kessy dk88, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Raphael Daudi/Juma Mahadhi dk75, Thabani Kamusoko, Ibrahim Hajib, Donald Ngoma na Emmanuel Martin.