Waziri
Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amevunja ukimya na kusema kwamba
watawala wanaendesha nchi kwa visasi ndiyo maana tangu ahame Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema)amezidi kuandamwa ikiwamo kunyang’anywa mashamba anayoyamiliki
kihalali.
Sumaye
ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Chadema, amesema
tangu ajiunge na upinzani amekuwa akikumbana na vikwazo vingi, ikiwamo
kudhauliwa pamoja na kuporwa mashamba yake kwa kisingizio kwamba
ameshindwa kuyaendeleza.
Amemtuhumu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kwamba
anajua ukweli kuhusu mashamba yake lakini hataki kuusema kwa kuwa
ametumwa na mkubwa wake.
Ametaja
mashamba aliyoporwa kuwa ni lile la Mvomero mkoani Morogoro na lililopo
Mabwepande katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambayo
yote serikali imefuta hati za umiliki wake.
Amesema
shamba la Mvomero linamilikiwa na mke wake Ester Sumaye ambalo lina
ukubwa wa hekari 326, na kwamba huko alikuwa anafuga ng’ombe zaidi ya
200, kondoo 300, ghala la kuhifadhia chakula, trekta na nyumba mbili za
kudumu.
Sumaye
akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za makao makuu
kanda ya Pwani (Chadema) , amesema mgogoro huo ulianza mara baada tu
ya yeye kuhamia upinzani.
Amesema
muda wote aliokuwa ndani ya CCM, hakuwahi kuwa na mgogoro wowote na
serikali wala kusumbuliwa kuhusu mali zake yakiwamo mashamba.
“Mara baada tu ya mimi kuhama wapo viongozi waliodiriki kusema huyu
Sumaye dawa yake ni kumfilisi kwa kumnyang’anya mashamba, kama moja ya
kunikomoa tu, hivyo ni dhahiri kuwa ni uadui kati ya serikali na mimi
kwa sababu ya kuhamia upinzani.” amesema Sumaye.
“Mashamba
hayo wanadai wameamua kuninyang’anywa kwa kuwa siyalipii kodi na
kutoendelezwa hivyo yanatakiwa kuchukuliwa na kuwagawia wananchi kitu
ambacho si weli kwani shughuli za kilimo katika mashamba hayo zilikuwa
zikiendelea kama kawaida.”
Sumaye
amemtaka, Lukuvi kutumia nafasi yake vizuri kwani kwa kuendeleza uadui
wa kisiasa hakuwezi kulisaidia taifa badala yake kutazidi kukandamiza
demokrasia hapa nchini.
Sumaye
ameionya serikali ya awamu ya tano na kuitaka iache kulipa visasi kwa
wapinzani na kuwatahadharisha watawala kwamba dhambi itawatafuna kwani
wapo viongozi wengine wa CCM wana mali nyingi na mahoteli makubwa kuliko
shamba lake lakini hawaguswi.