Mhashamu Anthony Mayala.
Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Anthony Mayala, anazikwa leo jimboni humo, wakati waumini wa Kanisa Katoliki jimboni humo na wenzao kote Tanzania wanaendelea kuomboleza kifo cha Askofu huyo aliyeaga dunia wiki iliyopita katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, kwa ugonjwa wa moyo.
Katibu Mtendaji wa Idara ya Habari ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Revocatus Makonge, alisema kuwa kikao cha kupanga mazishi hayo kimefanyika jimboni humo na kwamba kikao hicho kiliwashirikisha mapadri na maaskofu kadhaa akiwamo Rais wa TEC, Askofu Yuda-Thadeus Ruwaichi, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, na Askofu wa Jimbo la Tabora, Paul Ruzoka.
Padri Makonge alisema ibada ya misa ya maziko hayo itafanyika katika viwanja vya Kawekamo Kanisa Kuu la Epfania Bugando. Alisema, misa hiyo inatarajiwa kuongozwa na Kardinali Pengo kwa kushirikiana na maaskofu wengine kutoka majimbo ya Kanisa hilo nchini.
Kwa kawaida ya Kanisa hilo, maaskofu huzikwa ndani ya Kanisa Kuu la Jimbo, hivyo Askofu Mayala atazikwa ndani ya Kanisa la Epfania.
BLOG HII INATOA POLE KWA WAKRISTO WOTE PAMOJA NA WOTE WALIOGUSWA NA MSIBA HUO KWA NAMNA MOJA AU NYINGINE.!!!!!