Ahadi ya Rais John Magufuli kuwa ataunda
Baraza dogo la Mawaziri imejenga shauku ya Watanzania kufahamu kiwango
cha ukubwa au udogo wa baraza hilo ikilinganishwa na mabaraza
yaliyoundwa na watangulizi wake baada ya kuapishwa, tangu Tanzania ipate
Uhuru mwaka 1961.
Baraza hilo la Dk Magufuli ambalo Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema litatangazwa muda ukifika,
tayari limechukua muda mrefu zaidi kuandaliwa, ikilinganishwa na
mabaraza ya kwanza ya marais waliomtangulia tangu kuanza kwa mfumo wa
vyama vingi vya siasa nchini.
Changamoto inayomkabili Rais Magufuli ni
kuunda baraza litakalokidhi matarajio yake na kauli mbiu yake ya “Hapa
ni Kazi Tu” na matarajio ya Watanzania kwa upande mmoja na ahadi yake
kwa upande mwingine, ya kuwa na baraza dogo.
Akilihutubia Bunge mjini Dodoma hivi
karibuni na wakati akiwa katika mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi
Mkuu, Dk Magufuli aliahidi kuunda baraza dogo ikiwa ni njia za kudhibiti
matumizi ya Serikali kwa nia ya kutafuta majawabu ya kero za wananchi
kwa kasi inayostahili.
Kutokana na ahadi yake, jambo ambalo
halitarajiwi ni Dk Magufuli kuteua mawaziri, idadi sawa na alioanza nao
mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete aliyevunja rekodi ya kuunda Baraza
kubwa kuliko marais wote waliomtangulia tangu Uhuru.
Baraza hilo alilounda Kikwete mwaka 2005
baada ya kuingia madarakani, lilikuwa na mawaziri 60, kati yao 29
walikuwa mawaziri kamili na 31 naibu mawaziri.
Kinyume chake, Serikali ya Awamu ya
Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndiyo iliyovunja rekodi
ya kuwa na Baraza dogo la mawaziri 11 mwaka 1961.
Katika awamu ya pili mwaka 1985, Rais
Ali Hassan Mwinyi alipoingia madarakani aliunda Baraza la Mawaziri lenye
mawaziri 23 na manaibu wanane, jumla walikuwa 31.
Mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa alianza na mawaziri 27 na naibu mawaziri 10, jumla walikuwa 37 na aliowaita askari wa miamvuli.
Kauli ya wasomi
Wachambuzi wa masuala ya siasa na
utawala wanapendekeza kuwa kutokana na mahitaji ya sasa na jitihada za
kubana matumizi, Baraza lingefaa kutozidi mawaziri 20.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk Benson Bana alisema ukubwa au udogo wa baraza unategemea na
vipaumbele vya Rais katika kipindi chake cha uongozi kama vitakidhi
mahitaji ya Watanzania.
“Haiwezekani kuwa na wizara 10 au chini
ya hapo kutokana na ukubwa wa nchi na utendaji kazi wa Serikali kwa
sasa, lakini sidhani kama kuna haja ya kuzidisha zaidi ya wizara 20,”
alisema.
Kauli hiyo imeshabihiana na aliyoitoa
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho kuwa
kulingana na mahitaji ya wananchi kwa sasa, hakuna haja ya kuwa na
wizara zaidi ya 22.
Alisema udogo wa baraza hilo utategemea na namna ambavyo Rais Magufuli atapunguza na kuunganisha wizara zisizokuwa na uzito.
“Kuna wizara ambazo hata zikipunguzwa
hazina athari na zinaweza kuvunjwa au kuunganishwa kwa ufanisi zaidi,”
alisema. Mapendekezo ya wachambuzi hao yanaenda sanjari na yale
yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba Mpya ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo ibara ya 93(2) ilikuwa imependekeza Baraza la Mawaziri
lisizidishe watu 15.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilitupiliwa
mbali wakati wa kujadili rasimu hiyo katika Bunge la Katiba ambalo
lilifanikisha kuanzishwa kwa Katiba Inayopendekezwa inayosubiri kupigiwa
kura ya maoni.