Wabunge wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametajwa kukataa uteuzi
wa nafasi ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne zilizokuwa wazi,
imebainika.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya Rais Dk.
John Magufuli, ambaye aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12, mwaka huu.
Wabunge hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini walidai kuwa kasi ya Rais Magufuli inawatia hofu.
“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito na kwangu ni ngumu na
nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya taarifa hizi nasikia na
wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.
“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada ya kupima nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge wangu,” alisema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri, Desemba 10, mwaka huu, Rais
Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana na
sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo na kwamba anaendelea
kuwatafuta.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliteua manaibu waziri wa wizara
hizo, huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake baadaye
atakapomaliza mchakato.
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi
Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo naibu wake ni
Dk. Ashatu Kijaji.
Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii, ambayo naibu wake ni Mhandisi
Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma,
Stella Manyanya.