Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ameapishwa jana na Rais Dkt.John Magufuli kushika wadhifa huo amewaomba wadau na wananchi kwa
ujumla kumpa muda.
Akiongea
na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa, Dkt. Mwakyembe
ambaye alikuwa waziri wa wizara mbalimbali katika serikali ya awamu ya
nne amesema kuwa anafahamu changamoto nyingi katika mfumo wa sheria ya
nchi akiwa kama mwananchi. Hivyo, ameomba kupewa muda ili atakapoingia
ofisini azifanyie kazi changamoto hizo.
Dk.
Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliyebobea, alieleza kuwa
mfumo bora wa sheria ya nchi ni kitu muhimu katika kipindi hiki ambacho
serikali imeamua kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo.
“Tuko
katika kipindi cha mageuzi makubwa ya uchumi wetu na masuala ya kijamii
na kiuchumi, kwahiyo masuala ya kisheria yatajitokeza sana hapo. Ndio
maana nasema… sawa ni eneo langu kisheria lakini changamoto ziko nyingi
ambazo lazima tukabiliane nazo ili nchi yetu iende kwa kasi ambayo Rais
wetu ameanza nayo,”amesema.
Akizungumzia
mchakato wa Katiba Mpya uliokuwa ukiendelea katika serikali ya awamu ya
nne, Dk. Mwakyembe amesema suala hilo litakamilishwa kutoka pale
lilipoishia.
“Mheshiwa Rais ameshalielezea vizuri sana hilo kwamba katika kipindi chake
tutalifanyia kazi, na hatukuishia pabaya tuliishia pazuri tu,
tutalitekeleza, muda utafika na naamini tutalikamilisha vizuri
tu,”aliongeza.