Sakata ya usajili wa nahodha wa timu
ya soka ya Tanzania, Mbwana Samatta inaonekana kukamilika baada ya
mshambulizi huyo kukubali kujiunga na klabu ya ubelgiji ya KRC Genk.
Samatta maarufu Samagoal, ameanza safari ya kuelekea Ubelgiji ambapo anatarajiwa kusaini mkataba na klabu hiyo.
Ajenti
wa nyota huyo, Jamal Kisongo ametetea hatua ya Samatta kujiunga na Genk
licha ya Nantes kutoa donge nono Zaidi ya Genk huku akisema kuwa uamuzi
huo ni kwa minajili ya ufanisi wa Samatta.
''Wachezaji wengi
waTanzania wanaazimio la kucheza soka Ulaya na naamini fursa hiyo
itafika kwani hali ya sasa itafungua milango kupitia Genk''.
Kisongo
ameongeza kuwa mkataba huu mpya na Genk utawanufaisha pia wachezaji wa
Tanzania kwani makubaliano hayo yataiwezesha klabu hiyo kusaka vipaji
zaidi nchini Tanzania.
Samatta ambaye pia ni mchezaji bora wa
wachezaji wa nyumbani barani Afrika anatarajiwa kupigania nafasi yake ya
kikosi cha kwanza cha Genk.
''Ni muhimu kwa Samatta kuingia na
kucheza katika kikosi cha kwanza cha Genk na inatarajiwa hali hio
itamwezesha kutimiza ndoto hiyo,'' alisema Kisongo.
Uhamisho wa
Samatta unadaiwa kuzua utata baina yake na mmiliki wa klabu ya TP
Mazembe, Moise Katumbi kwani Katumbi alichagua Nantes ambayo ilitoa
kitita bora zaidi.
-Samatta aliichezea Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mnamo mwaka wa 2011.
-Aliisaidia TP Mazembe kutwaa taji la vilabu bingwa barani Afrika.
-Alituzwa mchezaji bora Afrika.