Rais wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini Sylvester Ambokile kupisha uchunguzi katika idara ya uhamiaji.
Taarifa
kutoka kwa kaimu mkurugenzi wa mawasiliano ya ikulu Gerson Msigwa
imesema Bw Ambokile amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za rushwa,
ukusanyaji mbaya wa maduhuli ya serikali, ukiukwaji wa taratibu za
manunuzi na utendaji mbovu.
Tuhuma hizo zilibainika wakati waziri
wa mambo ya ndani ya nchi Bw Charles Kitwanga alipotembelea idara ya
uhamiaji hivi karibuni
Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na fedha Bw Piniel Mgonja pia amesimamishwa kazi.
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema watendaji hao wakuu wa
uhamiaji wamesimamishwa kazi mara moja hadi hapo uchunguzi
utakapokamilika.
“Endapo watabainika kutokuwa na makosa Rais ataamua hatima yao,” amesema.
Hayo yakijiri, Dkt Magufuli pia amemrejesha Bw Eliakim Chacha
Maswi kuwa katibu tawala wa mkoa wa Manyara, baada ya kuhudumu kipindi
kifupi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Bw Maswi alikuwa ameteuliwa kuwa kaimu naibu kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
“Rais
Magufuli amefanya mabadiliko hayo kwa lengo la kumtafuta mtu mwenye
utaalamu wa kuendeleza kazi iliyofanywa na Bw Maswi,” Bw Sefue
amenukuliwa katika taarifa hiyo kutoka ikulu.
Tangu kuchukua madaraka mwezi Novemba mwaka jana, Dkt Magufuli amewasimamisha au kuwafuta kazi maafisa wengi wakuu serikalini.