Rene Angelil alihudumu kama meneja wa Celine Dion hadi 2014
Rene Angelil, mume wa mwanamuziki
mashuhuri duniani Celine Dion, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka
73, mwanamuziki huyo ametangaza.
Bw Angelil, aliyemuoa Dion mwaka 1994 na wakajaliwa watoto watatu, amekuwa pia akihudumu kama meneja wake.
Alifariki akiwa nyumbani kwao Las Vegas baada ya kuugua saratani.
Dion
alichukua likizo kutoka kwenye muziki kwa vipindi viwili ili kumtunza
Angelil baada yake kupatikana na saratani ya koo mwaka 2000.
Bw Angelil alizaliwa mjini Montreal mwaka 1942.
Baada
ya kuwa meneja wa makundi kadha nchini Canada, aliombwa na wazazi wa
Dion awe meneja wake mwanamuziki huyo alipokuwa na umri wa miaka 12
pekee.
Mwaka jana, Dion aliambia gazeti la USA Today kwamba alikuwa akijiandaa kwa kifo cha mumewe.
“Ikifika, itafika tu,” aliambia gazeti hilo Agosti 2015.
“Lakini
kibarua change kikubwa kitakuwa kumwambia mume wangu kwamba tuko sawa.
Nitawatunza na kuwalea watoto wetu. Utatutazama kutoka ulimwengu
mwingine.”
Gazeti la Montreal Gazette linasema Bw Angelil aliweka
rehani nyumba yake ili kupata pesa za kufadhili albamu ya kwanza ya
mwanamuziki huyo.

Dion amerekodi albamu 25 studioni na ndiye mwanamuziki wa tano kwa
kulipwa pesa nyingi zaidi, utajiri wake ukikadiriwa kuwa $630m (£437m).
Mwaka 1999, wimbo wake My Heart Will Go On, uliotumiwa katika filamu ya Titanic, ulishinda tuzo mbili za Grammy.
Amekuwa akitumbuiza mara kwa mara katika ukumbi wa The Colosseum, Caesars Palace mjini Las Vegas tangu 2003.
Alianza
tena kutumbuiza mashabiki wake mwaka jana baada ya kupumzika mwaka
mmoja kumtunza Bw Angelil, ambaye aliacha kuwa meneja wake 2014.