
Waziri wa nchi, ofisi ya rais -tawala za mikoa na serikali za mitaa,
Tamisemi Mh. George B. Simbachawene amewasimamisha kazi wakurugenzi
watendaji wa manispaa za Kigoma, mkoa wa Kigoma na manispaa ya Mpanda,
mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kuridhia na kutekeleza maamuzi ambayo
yamesababishia serikali hasara na upotevu wa fedha.
Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Mhandisi Boniface Nyambele
anakabiliwa na tuhuma ya uuzaji wa nyumba za halmashauri bila kufuata
sheria, kanuni na taratibu zilizopo na bila kibali cha waziri mwenye
dhamana kama sheria inavyo elekeza.
Mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda ndugu Suleiman Lukanga ana
kabiliwa na tuhuma za ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa kiasi cha
shilingi milioni tisini na mbili na laki saba na elfu hamsini
(92,750,000/=) na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa skimu ya umwagiliaji
ya Kakese kiasi cha shilingi milioni mia mbili, tisini na nne
(294,000,000/=).
Aidha, Mheshimiwa waziri wa nchi ameagiza nafasi ya mkurugenzi wa
manispaa ya Kigoma ikaimiwe na Mhandisi Sultan Imari Ndilowa ambaye ni
mkuu wa idara ya maji, manispaa ya Kigoma, nafasi ya mkurugenzi wa
manispaa ya Mpanda ikaimiwe na ndugu Lauteri John Kanoni ambaye ni
katibu tawala msaidizi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa waziri wa nchi, amewataka wakurugenzi watendaji wa
mamlaka za serikali za mitaa kote nchini kuwa makini katika kutekeleza
majukumu yao wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote
ambao watakiuka matakwa ya sheria, kanuni na taratibu na kutoweka mbele
maslahi ya umma.