Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Agosti, 2017 amekutana
na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Japan (JICA),Bwana Shinichi Kitaoka Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika Mazungumzo hayo Bw. Kitaoka amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa
uongozi mzuri na wa mfano hususani katika kupambana na rushwa na
msukumo mkubwa anaoutoa katika maendeleo hususani katika kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Jitihada zinazosaidia kuimarisha uchumi
na kuboresha huduma za kijamii na kuahidi kuwa JICA itaendelea kuwa
mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania.
Bw. Kitaoka ambaye ni mara yake ya kwanza kuitembelea Tanzania kama
Rais wa JICA amemuahidi Rais Dkt Magufuli kuwa miradi yote ya maendeleo
ya nyuma na ya sasa inayotekelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania na JICA
itamalizika kwa wakati ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara za juu (
Flyover)
wa TAZARA unaoendelea kujengwa hivi sasa,mradi wa ujenzi wa barabara ya
Mwenge - Moroco yenye urefu wa kilomita 4 nukta 3 pamoja na mradi wa
ujenzi wa daraja la Gerezani.
“Tumefikia makubaliano mazuri kuhusiana na miradi
tunayoendelea kuitekeleza hapa nchini na wananchi watarajie kuona kazi
zikifanyika kuanzia mwezi june,mwakani hususani katika ujenzi wa daraja
la gerezani na mingineyo”
Kwa upande wake Mhe. Dkt Rais Magufuli amemshukuru Rais huyo wa
Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan Bw. Shinichi Kitaoka kwa
uamuzi wake wa kuja Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania inatambua
mchango mkubwa ambao Japan inautoa katika maendeleo ya Tanzania kupitia
JICA, na kwamba itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake
na Japan katika masuala mbalimbali.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru JICA kwa kutoa fedha kwa ajili ya
kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi jijini Dar es Salaam ikiwemo upanuzi
wa barabara ya Mwenge – Morocco, utakaoiwezesha barabara hiyo kuwa na
zaidi ya njia nane, ujenzi wa barabara ya TAZARA, ujenzi wa Daraja la
Gerezani njia nne, na barabara ya Bendera tatu hadi Kamata.
“Tunathamini sana mchango unaotolewa na walipa kodi wa
Japan kupitia JICA katika kutekeleza miradi ya maendeleo hapa nchini na
ninakuomba kuangalia uwezekano wa kufadhili na kujenga miundo mbinu na
miradi mbalimbali ya maendeleo katika Makao Makuu ya nchi Dodoma ambako
serikali imedhamiria kuhamia huko ili kuweka alama ya urafiki na
mahusiano mema yaliyopo kati ya Tanzania na Japan”
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe.
Masaharu Yoshida,Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango Doto James,
Katibu Mkuu Ujenzi Mhandisi Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Barabara nchini Mhandisi Patrick Mfugale.
Emmanuel Buhohela,
Mwandishi wa Habari,Msaidizi wa Rais,
Dar es Salaam.
21 Agosti, 2017