Waziri wa Ulinzi Dr. Hussein Mwinyi
TAARIFA KWA UMMA DODOMA, FEBRUARI 17, 2011Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imeeleza kushtushwa na kusikitishwa na taarifa za milipuko ya mabomu katika Ghala la Kuhifadhi Silaha la Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika eneo la Gongolamboto, Dar es Salaam jana jioni.
Aidha, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewapa pole ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Tanzania kwa sababu ya maafa haya. Pia Kambi hiyo imezitaka mamlaka zote za umma zinazohusika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wananchi wote walioathirika na maafa haya wanapatiwa huduma zote wanazohitaji katika kipindi hiki cha msiba huu. Hii ni pamoja na kuwapatia huduma za maziko wale wote waliofariki, matibabu kwa waliojeruhiwa na hifadhi kwa wale waliopoteza makazi yao. Aidha, ni muhimu kwa vyombo vya usalama kuhakikisha ulinzi wa mali za wananchi katika maeneo yote yaliyoathirika na ambazo zitakuwa hazina ulinzi baada ya wananchi kukimbia maeneo yao.
Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeeleza kwamba tukio hili ni la kushtusha na kusikitisha hasa kwa kuzingatia kwamba haijapita miaka miwili tangu tukio la aina hiyo hiyo litokee katika Ghala ya Silaha ya Kambi nyingine ya JWTZ katika eneo la Mbagala, Dar es Salaam, ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu thelathini na uharibifu mkubwa wa mali za umma na za wananchi binafsi. Aidha, milipuko ya Mbagala ilipelekea Serikali kutumia mabilioni ya fedha za umma kwa ajili ya malipo ya fidia kutokana na vifo, majeruhi na uharibifu wa mali binafsi za wananchi.
Akielezea tukio la milipuko ya Gongo la Mboto, Msemaji wa Ulinzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mh. Joseph Selasini alisema: “Milipuko ya Gongo la Mboto inaonyesha dhahiri kwamba Serikali ya Awamu ya Nne ya Chama cha Mapinduzi (CCM) haijajifunza lolote kutokana na maafa yaliyotokea Mbagala mwaka juzi. Maana kama Serikali ingejifunza kutokana na maafa hayo ingeshachukua hatua za dharura na za haraka kuhakikisha kwamba maafa ya aina hii hayatokei tena.” Mh. Selasini alizitaja baadhi ya hatua hizo kama ni pamoja na kuhamisha maghala yote ya silaha na mabomu yaliyo karibu na maeneo wanayoishi raia na kuyapeleka katika Kambi za JWTZ zilizoko mbali kabisa na maeneo ya raia. “Haiwezekani kwa Serikali kuendelea kuweka maghala ya silaha katika Kambi za Jeshi zilizo karibu na wananchi na hivyo kuhatarisha maisha yao namna hii”, alisema Mh. Selasini.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewataka Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dr. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange kujiuzulu mara moja ili kuwajibika kisiasa kutokana na maafa ya Gongo la Mboto na ili kupisha uchunguzi huru na wa kina wa chanzo na/au sababu za milipuko hiyo. Mh. Selasini alisema: “Dr. Hussein Mwinyi alikuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa maafa ya Mbagala; na Jenerali Mwamunyange alikuwa Mkuu wa Majeshi. Maafa ya Mbagala yalitokea chini ya dhamana na/au usimamizi wao. Na mara baada ya maafa hayo, Waziri Mwinyi na Jenerali Mwamunyange waliliahidi taifa kwamba maafa ya aina hii hayatatokea tena. Sasa yametokea. Inaelekea, kwa hiyo, kwamba ahadi yao ilikuwa sio ya kweli na/au hawakuhakikisha kwamba inafanyiwa kazi ili iwe ya kweli. Viongozi hawa hawana budi kuwajibika kwa hiari yao wenyewe au kuwajibishwa kama itahitajika.”
Mh. Selasini aliongeza kusema kwamba hadi leo hakuna taarifa yoyote rasmi iliyowahi kutolewa hadharani kwa wananchi na/au kwa wawakilishi wao Bungeni ya chanzo na/au sababu za maafa hayo. “Hadi leo hii wananchi na/au wawakilishi wao Bungeni hawajaambiwa kama kulikuwa na makosa ya makusudi na/au ya uzembe na/au kama hatua zozote za kinidhamu na/au za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya mtu yeyote kutokana na kusababisha na/au kuwajibika kwa maafa hayo. Jana maafa mengine ya aina hiyo hiyo yametokea tena na kwa kadri ya taarifa rasmi ya Serikali watu wengi wameuawa na wengi wengine kujeruhiwa na mali nyingi kuharibiwa. Kwa sababu hizo, huu ni wakati muafaka kwa Dr. Mwinyi na Jenerali Mwamunyange kuonyesha uadilifu wao kwa kujiuzulu nafasi zao ili kuwajibika kwa maafa haya.”
Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imependekeza iundwe Tume Huru ya Uchunguzi na/au Kamati Teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuchunguza kwa kina chanzo, sababu na madhara yote yaliyosababishwa na milipuko ya Gongo la Mboto. “Kwa kuzingatia historia ya uchunguzi wa milipuko iliyotokea Mbagala mwezi Aprili 2009, Tume Huru na/au Kamati Teule ya Bunge lazima itoe taarifa yake hadharani kwa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, alishauri Mh. Selasini.